1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Ujerumani yahimiza kukomesha kwa vivutio vya uhamiaji

6 Oktoba 2025

Mkuu wa Polisi ya Ujerumani, Dieter Romann, amesema uhamiaji haramu unaweza kudhibitiwa tu endapo serikali itapunguza vivutio vinavyowafanya wahamiaji kukimbilia nchini humo na kuimarisha ulinzi wa mipaka na urejeshaji.

Ujerumani Berlin 2023 | Rais wa Polisi wa Shirikisho, Dieter Romann, akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kuhusu ripoti ya mwaka 2022.
Tangu mwaka 2012, Mkuu wa Polisi wa Shirikisho: Dieter Romann (picha ya maktaba). Picha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

Mkuu wa Polisi wa Shirikisho la Ujerumani (Bundespolizei), Dieter Romann, amesema tatizo la uhamiaji usiofuata sheria haliwezi kutatuliwa kwa ukaguzi wa mipaka pekee, bali linahitaji mkakati mpana unaounganisha sera za ulinzi, makazi na urejeshaji wahamiaji.

Akizungumza na gazeti la Welt am Sonntag, Romann alisema: "Tunahitaji mpango wa jumla. Hasa ni lazima kupunguza vichocheo ambavyo nchi yetu inaweka, hadi kiwango cha chini kinachoruhusiwa kikatiba.”

Ameonya kuwa Ujerumani inapaswa kutoa ujumbe wa wazi kuwa haiwezi kupokea watu bila mipaka na kwamba huduma kwa wahamiaji lazima ziambatane na masharti ya wazi.

Kwa kufanya hivyo, alisema, wahamiaji watapoteza motisha ya kujitosa katika safari hatarishi kuingia Ulaya.

Romann aliongeza kuwa bila mkakati wa kisiasa wa pamoja unaounganisha utoaji wa visa, ulinzi wa mipaka, haki za ukaaji, huduma za kijamii, na urejeshaji, tatizo la uhamiaji litaendelea "kwa ukubwa uleule.”

Kwenye mpaka wa Ujerumani na Poland | Afisa wa Polisi wa Shirikisho akifanya ukaguzi.Picha: dts-Agentur/picture alliance

Wito kwa serikali kutekeleza sera kwa uthabiti

Romann alisisitiza kuwa Polisi wa Shirikisho wanaweza kufanya ukaguzi, kuwazuia wasafirishaji haramu na kurudisha wahamiaji, "lakini hawawezi kulitatua tatizo hilo peke yao.”

Alisema hatua madhubuti zinahitajika kutoka kwa wabunge na serikali yenye dhamira ya kweli kutekeleza maamuzi yake.

Akizungumzia suala la urejeshaji wahamiaji (Abschiebungen), Romann alifichua kuwa mwaka uliopita majimbo ya Ujerumani yaliwasilisha maombi ya kurejesha takriban watu 53,800 kwa Polisi ya Shirikisho.

Hata hivyo, kati ya idadi hiyo, zaidi ya maombi 33,600 yaliahirishwa kabla wahusika hawajafikishwa kwa maafisa wa uhamiaji.

Kati ya sababu kuu za kuchelewesha mchakato huo ni wahamiaji kutoweka siku ya safari au kuwasilisha vyeti vya ugonjwa ghafla.

Kwa sasa, alisema, Ujerumani ina zaidi ya watu 226,000 wanaotakiwa kurejea makwao, lakini kuna nafasi chini ya 800 pekee katika vituo vya mahabusu ya urejeshaji.

Mkutano na wenzake mjini Munich | Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Alexander Dobrindt (katikati), katika "Mkutano wa Uhamiaji wa Munich"Picha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Vizuizi vya kisheria vya vituo vya urejeshaji

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Shirikisho, Alexander Dobrindt (CSU), amekiri kuwepo kwa changamoto za kisheria katika kuanzisha vituo vya urejeshaji (Rückführungszentren) kwa waombaji wa hifadhi waliokataliwa katika nchi za tatu.

Baada ya mkutano wa kilele wa uhamiaji uliofanyika mjini Munich, Dobrindt alisema: "Tupo mwanzoni mwa mchakato huu. Tayari kumekuwa na majaribio kadhaa na tumekutana na vikwazo vya kisheria.”

Amebainisha kuwa bado kuna tofauti za maoni miongoni mwa mataifa ya Ulaya kuhusu utekelezaji wa mpango huo, lakini mazungumzo yanaendelea ili kupata suluhisho la pamoja.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhamiaji wa Umoja wa Ulaya, Magnus Brunner, amesema ni muhimu Ujerumani iendelee kushinikiza hatua thabiti, akiongeza kuwa: "Ni hali isiyokubalika kwamba sasa ni mtu mmoja pekee kati ya watano wanaotakiwa kuondoka Ulaya ndiye anayefanya hivyo kweli.”

Chanzo: wa/pgr (kna, afp, dpa, rtr)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW