Mkuu wa shirika la IAEA Yukiya Amano afariki.
22 Julai 2019Amano, raia wa Japan mwenye mri wa miaka 72, alikuwa ameshikilia wadhifa wa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo tangu mwaka 2009 kutoka kwa raia wa Misri, Mohamed El-Baradei. Aliliongoza shirika hilo la Umoja wa Mataifa kupitia kipindi cha diplomasia kali kuhusiana na mpango wa kinyuklia wa Iran huku akijaribu bila mafanikio kurejea kwa Korea Kaskazini kwenye mpango huo.
Wakati wa kipindi chake, Amano aliongoza kutiwa saini kwa mkataba wa kihistoria mnamo mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita makuu duniani: Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani, ambapo taifa hilo la Kiislamu lilikubali kusitisha mpango wake wa kinyuklia iwapo Marekani ingekubali kuiondolea vikwazo.
Lakini Amano anaondoka duniani wakati taharuki ya kimataifa na Iran ikiongezeka, tangu Rais Donald Trump kujiondoa katika mkataba huo mnamo Mei 2018.
Kipindi cha tatu cha kuhudumu kwa Amano kama mkuu wa IAEA kilipaswa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2021, lakini alikuwa anatarajiwa kutangaza nia yake ya kujiuzulu mapema kwa sababu ya hali yake ya kiafya.
Mnamo mwezi Septemba mwaka jana, afisi ya Amano ilitangaza kuwa alikuwa amefanyiwa utaratibu wa matibabu ambao haukuwa umetajwa. Tangu kurejea kwake kazini, alionekana kuwa dhaifu.
Amano alishika nafasi ya ukurugenzi mkuu, baada ya kuhudumu kama mjumbe mkuu wa kitengo cha udhibiti wa kuenea kwa silaha katika wizara ya mambo ya nje ya Japan.
Mnamo mwaka 2017, mataifa wanachama wa shirika hilo la kimataifa yalimuidhinisha kuhudumu kwa muhula wa tatu ambao ulitarajiwa kukamilika Novemba 2021.
Mfumo wa uongozi wa Amano
Amano alipendelea zaidi mashauriano na diplomasia katika juhudi ya kimataifa za kukabiliana na kufuatilia mpango wa kinyuklia.
Pia aliliongoza shirika hilo kupitia kipindi kigumu cha ajali ya nyuklia ya mwaka 2011 katika kinu cha umeme cha Fukushima nchini Japan uliosababishwa na mtetemeko wa ardhi na Tsunami.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, amemtaja Amano kama mtu aliyejitolea katika utaalamu na aliyekuwa tayari kila wakati kusaidia katika huduma ya jamii ya kimataifa bila upendeleo.
Balozi wa Argentina katika shirika hilo, Rafael Grossi, anawania kuurithi wadhifa huo wa Amano, na wajumbe wanasema kuwa mratibu mkuu wa shirika hilo, Cornel Feruta wa Romania, pia anatarajiwa kujitosa katika kinyang'anyiro hicho pamoja na wagombea wengine.
Huku kila mgombea akiwa na mfumo wake wa uoongozi, inatarajiwa kwamba hakutakuwa na mabadiliko makubwa katika shirika hilo kuhusu jinsi ya kushughulikia masuala yake makuu ikiwa ni pamoja na Iran na uwezekano wa kurejea kwa Korea Kaskazini iliyowafurusha wakaguzi wa shirika hilo mnamo mwaka 2009.
Kutokuwa na habari kuhusu ugonjwa wa Amano pia kuliashiria jinsi afisi yake inavyoshughulikia habari muhimu kwa ujumla, ambapo wajumbe kutoka mataifa wanachama walielezea mara kwa mara kutatizika kwao katika kupokea habari za siri kutoka kwa Amano na wafanyakazi wake kuhusu masuala kama vile sera zake kuhusu mkataba wa kinyuklia kati ya Irana na mataifa yenye ushawishi mkubwa.
Hata hivyo, daima Amano alisisitiza kwamba shirika lake lilikuwa la mfumo wa kiufundi na sio kisiasa na kutofautiana na mtangulizi wake, El-Baradei, aliyemtangulia ambaye aligongana na maafisa wa Marekani kuhusu Iran na mara nyingi hakulindwa katika kujadiliana masuala muhimu