Mkuu wa shughuli za ujasusi wa ndani Ujerumani aandamwa
13 Septemba 2018Nchini Ujerumani mkuu wa shughuli za ujasusi wa ndani, Hans-Georgi Maasen, anazidi kukabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu katika wakati ambapo anaandamwa na tuhuma mpya kuhusu madai ya tathmini aliyoitowa kuelekea chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachochukia wageni cha AFD. Chama cha Social Democrats kinamtaka ajiuzulu.
Amejikuta akishikilia nafasi ya juu katika vichwa vya habari baada ya kutafautiana moja kwa moja na kauli iliyotolewa na Kansela Angela Merkel katika kutowa tathmini yake juu ya maandamano ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia katika mji wa Chemnitz.
Merkel alilaani kwa sauti kali kabisa hatua ya kuandamwa wageni kufuatia kisa kilichoonekana katika mkanda wa video uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kupigwa kwa raia asiyekuwa na asili ya Kijerumani lakini Maasen alihoji moja kwa moja uhalali wa mkanda huo wa video akitilia mashaka alau sehemu moja iliyoonekana katika vidio hiyo. Wakosoaji wanasema madai yaliyotolewa na Maasen yameangukia mikononi mwa wanasiasa kali za mrengo wa kulia na wanatumia hoja zake alizotoa kujipatia umaarufu.
Na si hilo tu lakini pia yameibuka maswali kuhusu lengo hasa alilokuwa nalo mkuu huyo wa shughuli za ujasusi nchini Ujerumani katika kutowa mtazamo huo katika wakati ambapo pia siku kadhaa za nyuma kabla ya kauli yake alituhumiwa kwamba aliwahi kukutana na wanasiasa wa AfD kuwapa ushauri kuhusu jinsi wanavyoweza kuepuka kufuatiliwa au kuchunguzwa mienendo yao, japo madai hayo ameyapinga waziwazi.
Chama cha SPD ambacho ni mshirika mkuu katika serikali ya muungano ya Kansela Merkel kimemuonya Merkel na kundi lake kwamba huu ni wakati wa Maasen kutimuliwa. Lakini kilichoonekana leo ni kwamba Maasen alau amefanikiwa kuepuka kupoteza wadhifa wake hasa baada ya bosi wake ambaye ni waziri wa mambo ya ndani Horst Seehorfer kumkingia kifua kwa kusema kwamba Maasen ni mtu ambaye mara kwa mara amekuwa akichukua msimamo wa kupinga siasa kali za mrengo wa kulia.
"Na hiyo ndio sababu napenda kuweka wazi kwamba mwenyekiti Maasen bado ana uungaji mkono wangu kama rais wa shirika la ndani la Ujasusi''
Kiongozi wa tawi la vijana la chama cha SPD Kevin Kuehnert ameshasema kwamba kadhia ya Maasen huenda ikatishia kuendelea kwa serikali ya muungano.
Maasen kama mkuu wa shirika la BfV anaongoza shirika ambalo linahusika kukusanya na kutathmini taarifa za kijaasusi zinazohusu harakati za kutaka kuvuruga kanuni za kidemokrasia au kuhujumu maslahi ya Ujerumani.
Lakini si hayo tu, miongoni mwa majukumu ambayo yanapaswa kufanywa na shirika hilo kufuatia kadhia ya NSU ilikuwa pia ni kurudisha imani ya wananchi kuelekea taasisi hiyo inayotuhumiwa kutokishughulikia kitisho cha siasa kali za mrengo wa kulia. Na kwa hivyo matukio haya ya karibuni ya AfD na makundi ya wafuasi wa siasa za kizalendo yamefufua upya masuali yanayotilia mashaka uwazi wa chombo hicho wa kutoegemea upande wowote.
Mandishi: Saumu Mwasimba/AFPE/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef