1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika akutana na rais wa Urusi

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
3 Juni 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, Rais wa Senegal Macky Sall na rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat katika makazi yake kwenye mji wa pwani wa Sochi.

Russland AU Präsident Macky Sall trifft Präsident Wladimir Putin in Sochi
Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/AP Photo/picture alliance

Mwenyekiti huyo Umoja wa Afrika amemtaka Rais wa Urusi Vladimir Putin kutilia maanani mateso katika nchi za Afrika yanayotokana na uhaba wa nafaka na mbolea unaosababishwa na vita vya nchini Ukraine. Sall amesema kuzuiwa kwa bidhaa hizo katika bandari za nchini Ukraine kumeiathiri dunia hasa nchi za Afrika hata kama ziko mbali na kanda vinakofanyika vita lakini nchi hizo ni waathirika katika ngazi ya kiuchumi kutokana na vita hivyo. 

Kushoto: Rais wa Urtusi Vladimir Putin. Kulia: Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/AP Photo/picture alliance

Mwenyekiti huyo Umoja wa Afrika amesema ni muhimu kushirikiana kwa pamoja ili yote yanayohusu chakula, nafaka na mbolea yawe nje ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Urusi baada ya nchi hiyo kuivamia kijeshi Ukraine. Katika hotuba mbele ya waandishi wa habari, Putin hakutaja moja moja juu ya usafirishaji wa nafaka lakini alisema Urusi siku zote iko upande wa Afrika na sasa ina nia hasa ya kuimarisha ushirikiano wake na bara hilo.

Operesheni ya ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine na msururu wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi vimetatiza usafirishaji wa mbolea, nafaka ya ngano na bidhaa nyingine kutoka nchi hizo mbili, na hivyo kusababisha kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta, hasa katika mataifa yanayoendelea.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Metzel/Sputnik/AP/picture alliance

Bei ya nafaka barani Afrika imepanda kwa sababu ya kudorora kwa ununuzi wa nje wa bidhaa kutoka Ukraine, na hivyo kuzidisha athari za migogoro na mabadiliko ya hali ya hewa hatua inayozidhisha hofu ya kuongezaka kwa migogoro ya kijamii. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa  nchi za Afrika ziliagiza asilimia 44 ya ngano kutoka Urusi na Ukraine kati ya mwaka 2018 na mwaka 2020 na kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika bei ya ngano imepanda kwa karibu asilimia 45 hii ikiwa ni matokeo ya kuzuiwa usafirishaji wa nafaka na bidhaa zingine kutoka Ukraine na Urusi. Nchi jizo ndiyo wazalishaji wakuu wa nafaka na mbolea duniani.

Vyanzo: AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW