1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa WHO abadili msimamo kuhusu chimbuko la Covid-19

16 Julai 2021

Mkuu wa WHO amekiri kwamba ilikuwa mapema kuondoa uwezekano wa uhusiano kati ya Covid-19 na uvujaji wa kimaabara, na kuiomba China kutoa ushirikiano kwa wanasayansi wanaoendelea kutafuta chimbuko la virusi vya corona.

Schweiz Generaldirektor der Weltgesundheitsorganisation (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Christopher Black/WHO/REUTERS

Katika hatua ya nadra ya kuondokana na unyenyekeo wake wa kawaida kwa mataifa wanachama yenye nguvu, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema upatikanaji wa taarifa za wazi umekuwa changamoto kwa timu ya kimataifa iliyosafiri kwenda China mapema mwaka huu kuchunguza chanzo cha Covid-19.

Visa vya kwanza vya mambukizi ya binadamu vilitambuliwa katika mji wa China wa Wuhan.

Tedros aliwaambia waandishi wa habari kwamba shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa lenye makao yake mjini  Geneva, Uswisi, linaiomba China kuwa muwazi na kutoa ushirikiano hasa kuhusu taarifa, data zilizoombwa katika siku za mwanzo za janga hilo.

Tedros amesema watajadili na mataifa wanachama kuhusu awamu ya pili na kuelezea matumaini kwamba mataifa wanachama yatasaidia katika kutoa miongozo ya kushughulikia changamoto alizoziainisha.

Mlinzi akifanya ukaguzi kwenye geti la taasisi ya virusi ya Wuhan, ambako inashukiwa kirusi cha Corona kilianzia.Picha: Koki Kataoka/AP/picture alliance

Soma pia: WHO yasema janga la maambukizi ya corona kuwa la muda mrefu

"Kama mnavyojua, tumekamilisha awamu ya kwanza, na awamu ya kwanza imeonesha kupigwa hatua fulani, lakini kuna baadhi ya changamoto zinazopaswa kushughulikiwa," alisema Tedros na kuongeza kuwa, "moja ya changamoto hizo ni upatikanaji wa data, hasa data za mwanzoni mwa janga, data za wazi ambazo hazikutolewa."

Shinikizo kutoka China?

Mkuu huyo wa WHO alisema kulikuwepo na shinikizo la kuondoa dhana kwamba kirusi cha corona huenda kilitoroka kutoka maabara ya serikali ya China mjini Wuhan --katika matamshi yanayopingana na ripoti ya WHO ya mwezi Machi, iliyohitimisha kwamba hakukuwa na uwezekano kabisaa wa uvujaji wa maabara.

Nilikuwa mtaalamu wa maabara mimi mwenyewe, na ni daktari wa mifumo ya kinga, na nimefanya kazi kwenye maabara, na ajali za maabara hutokea," Tedros alisema. "Ni jambo la kawaida.

Soma pia: Wataalamu wa WHO watembelea maabara ya Wuhan

Katika miezi ya karibuni, wazo kwamba janga la covid-19 lilianzia kwa namna fulani katika maabara - na yumkini lilihusisha kirusi cha kutengenezwa, limepata nguvu, hasa baada ya rais Joe Biden kuamuru mwezi Mei kupitia upya upelelezi wa Marekani kutathmini uwezekano huo.

China imejibu kwa kishari, ikihoji kuwa majaribio yoyote ya kuhusisha chimbuko la covid-19 na maabara yalikuwa yanasukumwa kisiasa, na badala ikitoa nadharia kwamba huenda kirusi hicho kilianzia nje.

Katika mkutano wa kila mwaka wa mawaziri wa afya wa WHO msimu wa machipuko, China ilisema kuwa utafutaji wa baadae wa chimbuko la Covid-19 unapaswa kuendelea katika mataifa mengine.

Wanasayansi walio wengi wanashuku kwamba kirusi cha corona kilitoka kwenye popobawa, lakini njia hasa kilimopitia kwenda kwa binadamu - kupitia kiungo cha mnyama au kwa njia nyingine - bado haijajulikana.

Kawaida huchukuwa muongo mzima kubaini njia ya asili ya kirusi cha mnyama kama Ebola au SARS.

Tedros alisema kwamba "kukagua kilichotokea, hasa katika maabara zetu, ni muhimu" ili kujiridhisha iwapo janga hilo lilikuwa na kiunganishi chochote cha maabara.