1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa wilaya Rwanda akamatwa

24 Julai 2017

Polisi Rwanda inamshikilia mkuu mmoja wa wilaya kwa tuhuma za kuwawekea vikwazo wagombea urais kwenye kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea kuelekea uchaguzi mkuu

Ruanda Wahlen
Picha: Picture alliance/Zumapress/G. Dusabe

Polisi nchini Rwanda inamshikilia mkuu mmoja wa wilaya kwa tuhuma za kuwawekea vikwazo wagombea urais kwenye kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini Rwanda. Polisi wanasema wanaendelea kufanya uchunguzi na kwamba kuna uwezekano wa kuwatia mbaroni watu wengine.

Hatua hiyo imefuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wapinzani kuhusu kusumbuliwa na viongozi wa ngazi za chini, baadhi ya wagombeaji hao walidai kukosa wafuasi wao mahali walipokuwa wakitazamiwa kufanya mikutano ya hadhara.

Na hii ndiyo awali ilipelekea waziri wa serikali za mitaa Francis Kaboneka, kuonya kuwa zitachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kiongozi wa ngazi za mwanzo atakayebainika kundeleza vitendo hivyo. Waziri Kaboneka anaendelea kusema kuwa: "Ni lazima watoe nafasi kwa wagombeaji kunadi sera zao kwa wapiga kura, labda nichukue nafasi hii kuwaonya viongozi wote wa ngazi za mwanzo, kwamba yeyote anayefanya vitendo hivi kuvisitisha mara moja pia niombe ngazi za usalama kufanya upelelezi ili atakayebainika achukuliwe hatua."

Siku moja tu baada ya kauli hiyo, ikatangazwa kuwa mkuu wa wilaya ya Rubavu kusini magharibi mwa nchi Jeremiah Sinamenye na baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wilayani kwake na wilaya jirani wamekamatwa kwa tuhuma hizo hizo za kuwazuia wananchi kuhudhuria mikutano ya hadhara kwa wagombeaji wa urais hasa yule wa chama cha kijani Frank Habineza na mgombea binafsi Philip Mpayimana.

Mgombea urais wa chama cha Democratic Green Party Frank HabinezaPicha: Getty Images/S. Aglietti

Taarifa hii imethibitishwa na msemaji wa jeshi la Polisi kamishna msaidizi Theos Badege. "Ni kweli kuna mahali ilibainika kwamba baadhi ya watu walishindwa kuheshimu sheria za tume ya taifa ya uchaguzi, miongoni mwao ni mkuu wa wilaya ya Rubavu na mfanyakazi mmoja wa wilaya ambao wanashikiliwa na polisi kwa sasa,sheria itatathmini baadaye uzito wa kosa lenyewe lakini niseme tu kwamba kuna wengine kutoka wilaya za Musanze, Nyaruguru na Nyagatare ambao tunawashikilia kwa tuhuma hizohizo."

Kwa upande mwingine baadhi ya wagombeaji wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema kwamba baada ya zoezi hili sasa wanaanza kuwapata wananchi wengi kusikiliza sera zao.

Msemaji wa jeshi la polisi ameonya kuwa uchunguzi unaendelea na yumkini kukawepo na watu wengine watakaotiwa mbaroni. Badege ameendelea kusema kuwa "Upelelezi unaendelea na tunasema kwamba yeyote atakayebainika na kosa hilo bila kujali atachukuliwa hatua za kisheria."

Hii ni siku ya kumi na moja ya kampeini za uchaguzi wa Urais utakaofanyika mnamo tarehe 4 mwezi ujao wa nane.Lakini kulingana na kampeini hizi Rais Paul Kagame wa chama tawala anayegombea muhula wa tatu anatarajiwa kushinda kwa urahisi.

Mwandishi: Sylvanus Karemera- DW Kigali

Mhariri: Saumu Yusuf