1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwamo kuhusu mkataba wa nyuklia wanufaisha pande husika

15 Agosti 2022

Iwe Iran au Marekani zitakubali au kukataa pendekezo la mwisho la kuufufua mkataba wa nyuklia wa Iran, wadadisi wasema kuuweka hai kunasaidia maslahi ya pande zote mbili.

Iran Teheran | Borrell Hoher Vertreter der EU und Außenminister Abdolahian
Picha: ATTA KENARE/AFP

Iwe Iran au Marekani zitakubali au kukataa pendekezo la mwisho la kuufufua mkataba wa kimataifa wa 2015 wa nyuklia wa Iran, hakuna upande unaoweza kusema mktaba huo umekufa kabisa kwa sababu kuuweka hai kunasaidia maslahi ya pande zote mbili. Hayo ni kulingana na wanadiplomasia, wachambuzi na maafisa ambao hata hivyo sababu wanazotoa ni tofauti sana.

Kwa utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani, hakuna njia nyingine ya wazi au rahisi kuudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran, isipokuwa njia ya makubaliano, ambapo Iran ilizuia mpango wake wa atomiki kufuatia makubaliano kwamba Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa zitaondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi yake.

Kwa kutumia shinikizo za kiuchumi kuishawishi Iran kuzuia zaidi mipango yake ya atomiki, kama ambavyo mtangulizi wa Biden, Donald Trump alivyojaribu baada ya kuitoa Marekani kwenye mkataba huo mwaka 2018, itakuwa jambo gumu wakati nchi kama China na India zinaendelea kununua mafuta kutoka Iran.

Iran yasema haina haraka kuyafufua makubaliano hayo

Ongezeko la bei ya mafuta kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, pamoja na hatua ya Moscow kuiunga mkono hadharani Iran, zimesaidia kuwapa maafisa wa Iran nguvu kiuchumi na kisiasa kwamba ufufuaji wa mkataba huo hakika unaweza kusubiri.

Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa jina amesema pande zote zinafurahi kuhusu hali iliyoko. "Hatuna haraka yoyote. Tunauza mafuta yetu, tuna bishara ya kutosha n anchi nyingi zikiwemo nchi jirani, tuna marafiki kama Urusi na China ambao wote hawaelewani vyema na Marekani… mpango wetu wa nyuklia unaimarika. Ni kwa nini turudi nyuma?'

Wakati Trump alipoitoa nchi yake kwenye mkataba huo, alidai kwamba ulipendelea sana Iran, hivyo alirudisha vikwazo vikali vya Marekani vilivyokusudia kuyasonga mauzo ya mafuta ya Iran, kama sehemu ya kampeni ya ‘shinikizo la juu'.

Juhudi za kuufufua mkataba wa nyuklia wa Iran

Baada ya kusubiri kwa muda wa mwaka mmoja, Iran ilianza kuukiuka mkataba huo kwa kujilimbikizia urani zilizorutubishwa, kurutubisha urani hadi asilimia 60, kiwango ambacho ni zaidi ya makubaliano ya asilimia 3.67. Aidha ilianza kutumia vinu vya kisasa zaidi.

Mpicha inayoonesha kiwanda cha kurutubisha urani eneo la NatanzPicha: Alfred Yaghobzadeh/SalamPix/abaca/picture alliance

Baada ya miezi 16 ya mazungumzo ya awamu mbalimbali lakini yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran, huku Umoja wa Ulaya ukizuru kila pande, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya alisema mnamo Agosti 8 kwamba wametayarisha pendekezo la "mwisho', na wanatarajia majibu katika wiki chache zijazo.

Wanadiplomasia wa kikanda walisema Umoja wa Ulaya uliziambia pande husika kwamba unatarajia majibu kabla ya Agosti 15, japo hilo halijathibitishwa. Hakuna dalili za Iran kutaka kufuata au kukubali pendekezo hilo la Umoja wa Ulaya. Kwa upande mwingine, Marekani imesema iko tayari kuhitimisha mpango kulingana na mapendekezo ya Umoja wa Ulaya na kwamba ingali inadurusu pendekezo hilo kabla itoe jibu.

Mabadiliko katika mizani ya kisiasa

"Vita vya Ukraine, bei ya juu ya mafuta, ongezeko la mvutano kati ya Marekani na China; vimebadili mizani ya kisiasa. Kwa hivyo, muda si muhimu kwa Iran,” amesema afisa mwengine wa pili wa ngazi ya juu nchini Iran.

Baada ya miezi kadhaa ya kusema muda unayoyoma, maafisa wa Marekani wamebadili mtindo wakisema watatafuta makubaliano bila kutilia maanani muda wa mwisho, ilimradi yawe yanazingatia maslahi ya usalama wa taifa la Marekani

Henry Rome, mchambuzi wa shirika la Eurasi Group, amesema pande zote mbili MArekani na Iran zina sababu za lazima, kuweka matumaini ya mkataba huo hai, ingawa hakuna upande unaoonekana kuwa tayari kufanya makubaliano ambayo kwa kweli yangewezesha ufufuaji wake.

Rome ameongeza kwamba haijabainika wazi ikiwa viongozi wa Iran wameamua kutoufufua mkataba huo au kama wameshafanya uamuzi thabiti, lakini kwa vyovyote vile, kuendeleza hali ya sasa ni kwa manufaa ya masilahi yao

(RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW