1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwamo wa shughuli za serikali waendelea Marekani

25 Desemba 2018

Pande zote mbili za kisiasa nchini Marekani bado zinavutana kuhusu ujenzi wa ukuta anaotaka kujenga Rais Donald kwenye mpaka na Mexico hazijapata ufumbuzi jinsi fedha zitakavyotumiwa katika kuujenga ukuta huo.

Donald Trump
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Katika taarifa ya pamoja, viongozi wa chama cha Demokratik seneta Chuck Schumer na mwenzake, spika Nancy Pelosi, wamemlaumu rais Donald Trump kwa mkwamo huo katika shughuli za serikali na pia kwa kuitumbukiza nchi kwenye matatizo. Wamesema Trump alitaka shughuli za serikali zikwame lakini kwa sasa anaonekana hajui vipi atajiondoa kwenye sakata hilo.

Kwa upande wake Trump alijisifu kwamba angeweza kuzikwamisha shughuli za serikali kwa ajili ya kupigania ujenzi wa ukuta, lakini sasa anawalaumu wanachama wa Demokratik kwa kukataa kuiunga mkono kura iliyohitajika kupitisha muswada wa bunge juu ya kuridhia dola bilioni 5.7 anazotaka kwa ajili ya kujengea ukuta huo. Viongozi hao wa chama cha Demokratik wameelezea hasara kubwa iliyotokea kwenye soko la hisa la Wall Street pamoja na uharibifu uliosababishwa na hatua ya Trump ya kumuachisha kazi waziri wake wa ulinzi.

Ni mpaka hapo Trump, ambaye anataka kuujenga ukuta huo baina ya Marekani na Mexico, na wanachama wa chama cha Demokratik, ambao wanaipinga hatua yake hiyo watakapokubaliana, sehemu ya shughuli za serikali ya Marekani zitaendelea kufungwa.

Viongozi wa chama cha Democrats. Kushoto: Chuk Schumer. Kulia: spika Nancy PelosiPicha: picture-alliance/CNP/M. H. Simon

Leo tarehe 25 mwezi wa 12 ni siku ya Krismasi na mkwamo huo umeingia katika siku yake ya nne na wala hakuna dalili kuwa hali hiyo itafikia mwisho wake hivi karibuni.

Wabunge wengi wameondoka kutoka kwenye jiji la Washington kwenda kujiunga na familia zao wakati ambapo kusherehekea Krismasi, rais Trump amebakia katika ikulu baada ya kuahirisha mipango ya sherehe za Krismasi katika makazi yake ya Florida.

Trump aliwaambia waandishi wa habari katika ikulu siku ya Jumatatu aliposhiriki kwenye mahojiano ya simu ambao ni utamaduni unaofanyika kila mwaka unaowashirikisha watoto na safari hii sana walitaka kujua ni lini baba Krismasi atawafikia waliko?. Trump amesema hakuna chochote kipya isipokuwa anachojua ni kwamba Marekani inahitaji usalama katika mpaka wake.

Trump alikutana Jumatatu na waziri wake wa ulinzi Kirstjen Nielsen na viongozi wengine wa idara ya usalama huku mazungumzo yakiendelea nyuma ya pazia kati ya wawakilishi wa serikali pamoja na wa vyama vya Republican na Demokratik.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE

Mhariri:Yusuf Saumu

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW