1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwe wa Trump kushirikiana na FBI

26 Mei 2017

Jared Kushner yuko tayari kutoa taarifa kuhusiana na mawasiliano yake na Urusi kwa wachunguzi wa serikali wanaofuatilia kadhia kuhusu madai ya kuwepo uhusiano kati ya Urusi na kampeini ya uchaguzi ya Trump.

USA Jared Kushner Berater und Schwiegersohn von Donald Trump
Jared Kushner Mshauri na mkwe wa TrumpPicha: Getty Images/AFP/T. Coex

Mwanasheria wa Kushner, Jamie Gorelick, amesema mteja wake yuko tayari kutoa ushirikiano endapo atatakiwa kufanya hivyo, huku kukiweko taarifa kwamba shirika la upelelezi wa ndani nchini Marekani FBI linachunguza mikutano aliyoifanya Kushner mnamo mwezi Desemba na maafisa wa Urusi.

Taarifa iliyotolewa na mwanasheria wa Kushner imeeleza kwamba awali mteja wake huyo alijitolea kushirikiana na bunge na kutoa taarifa kuhusu kile anachokifahamu juu ya mikutano na Urusi na hivi sasa pia yuko tayari kufanya hivyo ikiwa atatakiwa kutoa maelezo katika tume yoyote ya uchunguzi kuhusu mafungamano yake na Urusi. Wakati huo huo mwenyekiti wa kamati ya bunge inayosimamia suala hilo amelitaka shirika la FBI kuzikabidhi nyaraka zote zinazohusiana na mawasiliano yote ya mkurugenzi wa zamani wa shirika hilo James Comey na ikulu ya Marekani, White House pamoja na wizara ya sheria ikiwemo nyaraka ambazo ni za tangu kiasi miaka minne ya nyuma wakati wa utawala wa rais Barack Obama.

FBI pamoja na kamati hiyo ya bunge sambamba na majopo mengine kadhaa ya bunge wanafanya uchunguzi kufuatilia madai ya kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 nchini Marekani pamoja na uwezekano wa kuwepo uhusiano kati ya nchi hiyo ya Urusi na Kampeini ya Trump. Ikumbukwe kwamba Trump alimfuta kazi Comey mkuu wa zamani wa FBI  Mei 9 wakati yakiibuka masuali mengi juu ya uchunguzi wa shirika hilo la FBI uchunguzi ambao kwa hivi sasa unasimamiwa na mshauri maalum Robert Mueller ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa shirika hilo la upelelezi la FBI.

Jared Kushner ni mume wa mtoto wa Donald Trump, Ivanka Picha: Reuters/K. Lamarque

Kushner ambaye ni mshauri muhimu kabisa katika ikulu ya White House alikuwa na mikutano mwishoni mwa mwaka jana na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei Kislyak na mfanyakazi wa benki raia wa Urusi Sergei Gorkov. Hata hivyo inaelezwa na duru zilizopo karibu na uchunguzi huo kwamba uchunguzi wa FBI haumaanishi kwamba Kushner ni mshukiwa wa uhalifu.

Mwenyekiti wa kamati ya kusimamia masuala ya uchunguzi wa bunge Jason Chaffetz alimwambia kaimu mkurugenzi wa FBI Andrew MacCabe kwamba anataka afikishiwe mawasiliano yote aliyowahi kuyafanya Comey na ikulu ya White House pamoja na idara ya sheria kuanzia Septemba mwaka 2013 wakati Comey alipochukua hatamu za kuliongoza shirika hilo la upelelezi FBI chini ya rais Obama. Kwa mujibu wa Chaffetz lengo lake kubwa la kuchukua hatua hiyo ni kutaka kufahamu kwa kina na kutathmini mawasiliano ya Comey na ikulu sambamba na ofisi ya mwanasheria mkuu.

Si hayo tu lakini awali Chaffetz pia alitaka akabidhiwe mawasiliano yote ya binafasi kati ya Comey na rais wa nchi Trump ingawa jana alijibiwa na chombo husika kwamba hawezi kukabidhiwa mawasiliano hayo kwa sasa kutokana na kuendelea uchunguzi unaosimamiwa na Mueller. Chaffetz lakini anasisitiza kwamba bunge na wananchi wa Marekani wana haki ya kufahamu kila kitu kupitia uchunguzi huru na kwahivyo FBI na Comey wanalazimika kukabidhi kwa khiari nyaraka hizo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba.

Mhariri: Joseph Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW