Mladic asomewa mashitaka 11 The Hague
3 Juni 2011Akiwa amevalia suti ya kijivujivu na uso wenye fadhaa, Jenerali Mladic aliingia mahakamani akisindikizwa na walinzi wawili. Dalili za kudhoofika zilikuwa wazi kwenye kiwiwili kilichochoka cha jenerali huyu, ambaye aliwahi kujuilikana kwa jina la "Mchinjaji wa Bosnia". Mladic aliivua kofia aliyokuwa amevaa alipokuwa akikaa kitako kwenye sehemu maalum aliyoandaliwa.
Mabishano baina yake na Jaji Alphons Orie, yalichukuwa muda mrefu, huku Mladic akibishania kila jambo katika hatua ya awali kuhusiana na mwenendo wa mashitaka dhidi yake, hasa akisisitiza kwamba hali yake ya afya hairuhusu kufuatilia kwa makini kesi dhidi yake.
"Mimi ni mgonjwa sana. Nimesikia alichokisema mwendesha mashtaka. Lakini nataka wakati zaidi kufikiria hicho alichokisoma. Kwa hivyo, nistahmilie kwanza." Alisema Mladic kwa sauti iliyotulia.
Hata hivyo, hatimaye Jaji Orie, aliweza kusoma muhtasari wa mashitaka dhidi ya Mladic.
"Kwa mujibu wa mashitaka, wewe, Ratko Mladic, unashitakiwa kwa mauaji ya maangamizi, uhalifu dhidi ya ubinaadamu, na uvunjaji wa sheria na taratibu za vita, katika maeneo na hali mbalimbali, ikiwemo kushirikiana na wengine kutekeleza hayo." Jaji Orie alisoma hati hiyo ya mashitaka.
Kwa takribani miaka 16, Mladic alikuwa akitafutwa kukabiliana na siku ya leo.
Mjini Srebrenica, ambako ndiko mauaji ya maangamizi ya wanaume na watoto wa kiume wa Kiislamu wapatao 8,000 yalikotokezea, wazazi na jamaa wa wahanga hao walikuwa wakiangalia kesi hii moja kwa moja kupitia televisheni.
Wengi wao walikuwa wakitokwa kwa machozi hasa pale Jaji Orie alipokuwa akitaja mtiririko wa matukio yanayotajwa kwenye kesi ya Mladic.
"Kutoka kipindi cha kuanzia tarehe 11 Julai mwaka 1995 hadi tarehe 1 Novemba 1995, Ratko Mladic alishiriki katika matukio ya kuwaua wanaume na watoto wa kiume na kuwahamisha kwa nguvu wanawake, watoto wadogo na wazee kutoka Srebrenica." Alisema Jaji Orie.
Jaji Orie amesema kwamba mashtaka yanaonesha Mladic na wenzake wengine, akiwemo, Radovan Karadzic, walikuwa viongozi wakuu wa mkakati ambao ulianza Oktoba mwaka 1991 hadi Novemba 1995 uliokuwa na lengo la kuwaondoa kabisa Waislamu wa Bosnia na Wakroatia wa Bosnia kutoka ardhi ya Serbia na Bosnia-Herzegovina.
Mladic anashitakiwa sambamba na Karadzic, ambaye alikamatwa tangu mwaka 2008, lakini Karadzic hakuletwa mahakamani leo hii. Hata hivyo, sehemu aliyowekwa Mladic ni ile ile anayokuwa anakaa Karadzic na aliyowahi kukaa Slobodan Milosovic. Milosovic alikuwa akijitetea mwenyewe mahakamani hadi alipokutwa na mauti ya ghafla hapo mwaka 2006.
Wote watatu: Mladic, Karadzic, na hapo mwanzo Milosovic, wanatuhumiwa kwa mashitaka 11 yanayohusiana na uhalifu dhidi ya binaadamu katika vita vya Balkan vya baina ya mwaka 1992 na 1995.
Mladic alitarajiwa kukubali au kukataa mashitaka dhidi yake na ameomba zaidi ya mwezi mmoja kupitia hati ya kurasa 37 yenye mashitaka dhidi yake. Jaji Orie alikubaliana na ombi hilo na Mladic amerudishwa kizuizini hadi kesi yake itakapotajwa tena tarehe 4 Julai, saa 4.00 asubuhi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman