1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlinda amani wa Malawi apewa tuzo ya UN

25 Mei 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa medali ya heshima kubwa kabisa ya Umoja wa Mataifa ya ujasiri kwa mlinda amani kutoka Malawi aliyemuokoa mwenzake mashariki mwa Congo

Demokratische republik Kongo UN Friedensmission Monusco
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Guteress alimuita marehemu Chancy Chitete shujaa wa "kweli", akisema ulimwengu hauna watu wengi wa aina hiyo, kabla ya kumkabidhi mjane wake, Lachel Chitete Mwenechanya, na Medali ya Kapteni Mbaye Diagne kwa Ujasiri Mkubwa.

Chitete ndiye mpokeaji pekee wa pili wa tuzo hiyo kubwa ya kulinda amani, ambayo ilianzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka wa 2014. Medali ya kwanza ilitolewa 2016 kwa familia ya Diagne, muangalizi wa kijeshi wa Umoja wa Mataifa aliyewaokoa mamia ya watu nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994, kabla ya kuuawa.

Guterres amemtaja Chitete kuwa shujaa wa kweliPicha: Reuters/D. Balibouse

Guterres amesema kuwa wakati walinda amani wa Tanzania na Malawi walipokabiliwa na mashambulizi makali Novemba mwaka jana wakati wakifanya operesheni ya kuzuia mashambulizi kwenye miji miwili dhidi ya waasi wa ADF ambao walikuwa wakivuruga juhudi za kukabiliana na mripuko wa Ebola, "Chitete na kikundi chake walikaa imara na kutoa ulinzi kwa kujibu mashambulizi."

Hatua hiyo iliwawezesha "wale waliokuwa hatarini kusonga katika eneo salama," alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. Lakini kabla ya Chitete kuondoka, "akamuona mlinda amani wa Kitanzania aliyekuwa amejeruhiwa vibara, Koplo Ali Khamis Omary, aliyekuwa amejilaza asijue la kufanya wakati waasi wakikaribia."

"Chitete alifahamu kuwa alilazimika kuchukua hatua, au mwenzake alikuwa na uhakika wa kufa," alisema Guterres. "Alimburura Koplo Omary kumuweka katika eneo lenye usalama mzuri wakati risasi zikiendelea kufyatuliwa." Wakati Chitete alikuwa akimlinda mwenzake na kumpa huduma ya kwanza, alipigwa na risasi ya waas, alisema katibu mkuu. Chitete na Omary walihamishwa kwa ajili ya matibabu. "Koplo Omary alinusurika," Alisema Guterres. "Chitete hakunusurika."

"ushujaa usio wa ubinafsi wa Chitete na kujitolea uliwasaidia walinda Amani kutimiza lengo lao na kuliondoa kundi hilo la waasi kutoka ngome yake na hiyo ilikuwa muhimu kwa mapambano dhidi ya Ebola kuendelea," alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Omary, ambaye hakuwa katika hafla hiyo ya Ijumaa, alimsifu rafiki yake na "ndugu wa kuaminika wakati wa shida” katika hotuba baada ya kifo chake, akisema "Nina deni kubwa sana la Chitete kwa kuhatarisha maisha yake ili kuniokoa.”