Mmkutano wa G20 kujadili mzozo wa kanda ya euro
14 Oktoba 2011Lengo kuu la mkutano huo ni kuandaa mkutano wa viongozi wa taifa na serikali wa kundi hilo la G20 utakaofanywa mwezi wa Novemba mjini Cannes. Lakini, mkutano wa leo utashughulikia pia mzozo wa kanda ya euro unaohusika na Ugiriki na madeni ya nchi zingine za kanda ya euro. Mzozo wa kanda ya euro unazidi kuathiri ukuaji wa kiuchumi duniani, kwa hivyo ni matumaini ya mawaziri wa nchi zilizo nje ya Ulaya katika kundi hilo la G20, kuwa washirika wenzao barani Ulaya watathibitisha kuwa kila kiwezekanacho kinafanywa kuudhibiti mzozo huo. Wasiwasi ukizidi kuathiri maeneo mengine duniani, mawaziri wanaotoka nje ya Ulaya wanatazamiwa kuzungumza waziwazi kuhusu mzozo wa kanda ya euro.
Waziri wa Fedha wa Canada Jim Flaherty tayari alifanya hivyo hapo jana kabla ya kuondoka Ottawa kuelekea Paris. Yeye alisema, mzozo huo haushughulikiwi vya kutosha na kanda ya euro. Kuna hatari ya mtengano kutokea katika mkutano wa leo huku nchi za Ulaya zikikosolewa na mataifa mengine kuwa zinashindwa kuudhibiti mzozo wa madeni ulioanza tangu miezi kumi na nane iliyopita. Hiyo ni kinyume kabisa na mwaka 2009, ambapo nchi za G20 zilishirikiana kuanzisha mradi uliolenga kuufufua uchumi duniani.
Ujerumani na Ufaransa zinachukua muda kukubaliana njia ya kuongeza mitaji ya benki. Vile vile nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa katika kanda ya euro, zinatofautiana katika suala la kudhamini hati za pamoja katika kanda ya euro, kwani Ujerumani haitaki kuongeza mzigo wa madeni yake. Hata hivyo kiini cha mpango wo wote ule, ni makubaliano kuhusu njia ya kuuimarisha mfuko wa msaada wa dharura EFSF, kwa nchi zilizokumbwa na madeni. Kwa maoni ya mkuu wa masuala ya uchumi na fedha wa Umoja wa Ulaya, Olli Rehn,sekta ya binafsi pia inapaswa kusaidia. Amesema:
"Ni muhimu kwa sekta ya binafsi pia kubeba sehemu ya mzigo huo, kama serikali na wanalipa kodi wanavyofanya kwa kudhamini mikopo kwa ajili ya Ugiriki."
Wataalamu wa Ujerumani na Ufaransa wapo mbioni kutayarisha mswada wa dharura kabla ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya hapo Oktoba 23. Mzozo wa kanda ya euro umesababisha thamani ya hisa kuporomoka katika masoko ya fedha. Wawekezaji pia hawana tena imani na masoko ya fedha kwa sababu ya wasiwasi juu ya uwezekano wa Ugiriki na hata nchi zingine kufilisika.
Njia ya kupambana na ukosefu wa usawa katika uchumi wa dunia, jitahada za kufanya mageuzi katika mfumo wa sarafu duniani na kuanzisha sheria za kudhibiti biashara za fedha zinazopindukia viwango pamoja na taasisi za fedha, ni mada zilizo katika ajenda ya mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20 unaoanza leo jioni mjini Paris.
Mwandishi: Martin,Prema rtrd/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef