1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnada wa vitalu DRC wakinzana na malengo ya hali ya hewa

28 Julai 2022

Mnada wa vitalu vya mafuta nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unakinzana na malengo ya hali ya hewa ya bara la Afrika.

Demokratische Republik Kongo | Congo River
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaviweka mnadani vitalu 30 vya mafuta na gesi vilivyopo katika msitu wa Bonde la Kongo, kunakopatikana pia eneo kubwa zaidi la kitropiki. Udongo wa eneo hilo huchukuliwa kama "hifadhi ya hewa chafu ya kaboni" ambayo ikiwa itapenya na kutapakaa angani, basi kuna hatari mfumo wa ikolojia unaweza kutatizika.

Baadhi ya vitalu au maeneo yanayokodishwa kwa shughuli za mafuta, yanapatikana katika eneo la kwanza la uhifadhi barani Afrika, ambayo ni Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga, iliyoundwa mnamo mwaka 1925 na inayochukuliwa na Shirika la Kimataifa la UNESCO, kuwa urithi wa dunia na ngome iliyosalia ya sokwe wanaoishi kwenye milima.

Picha: Frans Lanting/picture alliance

Wanaadamu na wanyama hatarini

Bonde la Kongo lina ukubwa wa hekari milioni 530 katika eneo la Afrika ya kati na linawakilisha asilimia 70 ya ardhi yenye misitu katika bara zima la Afrika. Ni eneo la makaazi ya maelfu ya aina mbalimbali ya ndege na imehifadhi nyani wengi zaidi kuliko sehemu yoyote duniani, ikiwa ni pamoja na nyani wakubwa kama sokwe na Bonobos.

Si wanyama pekee, hata binaadamu pia wako hatarini. Jamii za watu wa Mbuti na Baka wanaweza kuhamishwa au hata kufukuzwa.

Soma zaidi: Congo kunadi haki za uchimbaji mafuta kwenye misitu ya mvua

Hatua ya Wizara ya nishati ya Kongo-Kinshasa imewakasirisha wanamazingira na wanaharakati wa hali ya hewa wanaosema kuwa uchimbaji mafuta utasababisha hatari kubwa kwa bara hilo ambalo tayari linakabiliwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi

Uchimbaji huo mafuta hatari kwa mazingira

Kituo cha Kimataifa cha utafiti wa Misitu kimeeleza katika utafiti wake kuwa, shimo kubwa katika eneo hilo na lililohifadhi hewa chafu ya kaboni, lina ukubwa wa kilometa za mraba 145,000, limehifadhi kiwango cha miaka 20 ya uzalishaji wa hewa ya kaboni inayotolewa na Marekani.

Soma zaidi:DRC kuendeleza juhudi za kuyalinda mazingira 

Maeneo mengine ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inapanga kuyaweka mnadani ni pamoja na vitalu vilivyopo kwenye Ziwa Kivu, Ziwa Tanganyika, na moja katika eneo la Mkoa wa pwani wa Albertine-Grabben, ambao ni upande wa magharibi wa mfumo wa Bonde la Ufa katika Afrika Mashariki.

Mnada huu wa sehemu ya msitu wa Bonde la Kongo, ambao unawakilisha asilimia 5 ya misitu ya kitropiki duniani, unajiri wiki moja baada ya Shirikisho la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira kufanya Kongamano mjini Kigali nchini Rwanda, kuhusu maeneo yanayohitaji kulindwa barani Afrika.  Huko, washiriki wa kongamano hilo, waliazimia kuimarisha ulinzi wa maeneo ya Afrika ambayo ni nguzo ya bioanuwai.

Mada zinazohusiana: 

Juhudi za kuzuwia kupotea kwa misitu asilia ya Kongo

02:44

This browser does not support the video element.

Eneo hilo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambalo ni hifadhi kuu ya hewa ya kaboni, liko hatarini kutokana na ukataji miti kiholela, upanuzi wa kilimo na mipango ya kubadili muelekeo wa maji ya Mto Kongo kuelekea katika Ziwa Chad.

Mwaka jana katika mkutano wa tabia nchi wa Umoja wa Mataifa wa COP26, wafadhili kadhaa waliopewa jina "Azimio la Viongozi wa Glasgow juu ya Misitu na Matumizi ya Ardhi",  waliahidi takriban dola bilioni 1.5 zitakazosaidia kufanya kazi kwa pamoja ili kusitisha uharibifu wa misitu na ardhi ifikapo mwaka 2030.

(AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW