Mnangagwa anusurika jaribio la mauaji
23 Juni 2018Msemaji wake, George Charamba, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba rais huyo mwenye umri wa miaka 75, ambaye kwenye mkutano huo alikuwa ameambatana na makamu wake wawili, yuko salama kwenye ikulu ndogo mjini humo.
"Rais ameondoshwa akiwa salama. Yuko kwenye nyumba ya serikali ya Bulawayo. Tunashukuru kwamba ulikuwa ni mripuko, na kwa hakika ulitokezea karibu sana na jukwaa kuu," alisema Charamba.
Shahidi mmoja ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mripuko ulitokea muda mchache baada ya Mnangagwa kumaliza hotuba yake na wakati akiondoka jukwaani.
Picha zilizotumwa mitandaoni zinamuonesha kiongozi huyo akiwapungia mkono wafuasi wake, akinyanyua hatua kuondoka jukwaani na kuanza kutembea kutoka meza kuu, ambapo sekunde chache baadaye mripuko unasikika. Watu walipiga makelele na moshi mkubwa kushuhudiwa.
Televisheni ya serikali ambayo ilikuwa ikirusha moja kwa moja mkutano huo, ilikatisha ghafla matangazo yake.
Makamu wa Rais miongoni mwa majeruhi
Makamu wote wawili wa rais - Constantino Chiwega na Kembo Mohadi wamejeruhiwa, sambamba na maafisa kadhaa wa chama tawala cha ZANU-PF, huku duru za kisiasa nchini Zimbabwe zikisema kwamba mashambulizi hayo yalikuwa ni jaribio la mauaji dhidi ya Mnangagwa.
Mwandishi wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, aliripoti kushuhudia watu kadhaa waliojeruhiwa ingawa hakuweza kutaja idadi kamili.
Picha za televisheni zinaonesha mtafaruku ukitokea, huku madaktari wakijaribu kuwaokoa waliojeruhiwa kwenye mripuko huo katika uwanja wa White City.
Mnagangwa alikuwa kwenye mji huo akijaribu kuwashawishi wapigakura kumchaguwa kwenye uchaguzi wa tarehe 30 Julai.
Huu utakuwa uchaguzi wa kwanza tangu mwanajeshi huyo wa zamani kumuondoa madarakani kwa mapinduzi baridi mshirika wake mkuu wa zamani, Robert Mugabe, mwezi Novemba mwaka jana baada ya kuwapo madarakani kwa miaka 37.
Uchaguzi huo utakuwa kipimo muhimu kwa Mnangagwa, ambaye ameahidi kuwa utakuwa huru na wa haki, katika wakati ambapo anaonekana kujaribu kujenga mahusiano mapya na jamii ya kimataifa.
Msemaji wa Rais Mnangagwa aliliambia gazeti la Zimbabwe Herald kuwa uchunguzi unaendelea, akisema kuwa kumekuwa na majaribio kadhaa ya kumuua rais huyo kwa kipindi kirefu.
Kama ilivyotokea Addis Ababa
Mripuko huo ulitokea masaa machache baada ya mwengine kama huo kutokea nchini Ethiopia, ambako mtu mmoja anatajwa kuuawa na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa, baada ya waziri mkuu mpya kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye mji mkuu, Addis Ababa.
Mripuko ulisikika muda mchache baada ya Abiy Ahmed kumaliza hotuba yake katikati ya Addis Ababa, na kuwasababishia watu kukimbia kunusuru maisha yao. Waziri mkuu huyo aliwahiwa kukimbizwa akiwa salama.
Awali Abiy alikuwa ameliambia shirika la habari la FBC kuwa "watu wachache wameuawa na ni mashahidi wa upendo na amani," lakini taarifa za baadaye kutoka ofisi yake zilisema hakuna aliyepoteza maisha kwenye mripuko huo.
Waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 42 alisema mripuko huo "yalikuwa mashambulizi yaliyopangwa vyema lakini yaliyoshindwa." Hata hivyo, hakurusha lawama zake kwa kundi lolote, ingawa alisema polisi wanaendelea na uchunguzi, akiongeza kuwa "mashambulizi hayo yalikuwa ya kitoto na yasiyokubalika. Daima mapenzi yatashinda. Kuwauwa wengine ni kushindwa. Kwa wale wanaojaribu kutugawa, nataka kuwaambia kuwa hamujafanikiwa."
Mripuko huo kwenye Uwanja wa Meskel uliokuwa umejaa watu mjini Addis Ababa, ulitokea baada ya wiki kadhaa za mageuzi makubwa kabisa ambayo yamewashitua wengi kwenye taifa hilo la pili kwa idadi ya watu barani Afrika, na baada ya miaka kadhaa ya hasira kali dhidi ya serikali, hali ya hatari, watu kukamatwa ovyo na kufungiwa kwa huduma za intaneti.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Sylvia Mwehozi