Modi aitangaza India kama kitovu cha Akili Mnemba duniani
19 Februari 2026
Modi ameyasema kwenye mkutano uliowakusanya baadhi ya viongozi wa dunia, wakuu wa makampuni ya teknolojia na watunga sera katika Mkutano wa Kimataifa wa Akili Mnemba mjini New Delhi. "India inaamini kwamba teknolojia ya akili mnemba itakuwa na manufaa tu wakati inaposambazwa na mifumo yake ya msingi ikiwa wazi; hapo ndipo mamilioni ya vijana wetu wataweza kuifanya iwe bora na salama zaidi."
Matamshi ya Modi yamejiri huku India — ambayo ni moja ya masoko ya kidijitali yanayokua kwa kasi zaidi — ikitaka kutumia uzoefu wake katika kujenga miundombinu mikubwa ya umma ya kidijitali na kujionyesha kama kitovu chenye gharama nafuu cha uvumbuzi wa teknolojia ya akili mnemba.
Mkutano huo pia ulihutubiwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mkurugenzi Mtendaji wa Google Sundar Pichai na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. Wametoa wito wa kuundwa mfuko wa dola bilioni 3 wa kuzisaidia nchi maskini kujenga uwezo wa msingi wa AI, ikiwa ni pamoja na ujuzi, ufikiaji wa data na uwezo wa vifaa vya kompyuta vya bei nafuu. India inautumia mkutano huo kujitanabahisha kama kiungo kati ya mataifa yaliyoendelea na nchi za ulimwengu wa tatu katika zama za Aikili Mnemba.