1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modi alaani mauaji ya watu kulinda ng'ombe India

29 Juni 2017

Waziri mkuu wa India Narendra Modi amelaani mkururo wa mauji ya watu wa jamii za wachache kwa kisingizio cha kulinda ng'ombe, ambao wanachukuliwa kuwa watakatifu na waumini wa madhehebu ya Kihindu.

Deutschland Berlin - Premierminister Narendra Modi
Picha: UNI

Kauli hiyo ya waziri mkuu ameitoa kufuatia ukosoaji dhidi ya serikali yake kwa kufumbia macho mauji hayo yanayofanywa na Wahindu wenye itakadi kali, na ameyatoa siku chache baada ya kijana wa Kiislamu kuchomwa visu hadi kuuawa akiwa kwenye treni baada ya kushutumiwa kwa kubeba nyama.

"Kuuawa watu kwa kutumia jina la Gau Bhakti (kuabudu ng'ombe) haikubaliki. Hili siyo jambo ambalo Mahatma Ghandi angeidhinisha," alisema Modi. India imekumbwa na wimbi la mauaji yanayofanywa na walinzi katika miezi ya karibuni, yakiwalenga Waislamu na Wahindu wa hadhi ya chini wanaotuhumiwa kwa kuuwa ng'ombe au kula nyama.

Siyo katika jina langu

Katika tukio la karibuni zaidi lililovutia nadhari, kijana Junaid Khan mwenye umri wa miaka 15 na ndugu zake watatu walishambuliwa wiki iliopita katika ugomvi ulionekana kama wa nafasi za kukaa kwenye treni wakati wakisafiri kwenda nyumbani wakitokea mjini New Delhi. Polisi imewakamata wanaume wanne kuhusiana na shambulio hilo.

Mwanaume akitembea katika ng'ombe katika mtaa mjini Varanasi. Mji huo uko kwenye kingo cha mto Ganges, ambao unachukuliwa kuwa mtakatifu na Wahindu.Picha: Getty Images

Mmoja wa ndugu zake Khan alisema washambuliaji waliwashutumu kwa kubeba nyama ya ng'ombe, ambayo ni maarufu sana miongoni mwa Waislamu wa India, lakini inaepukwa na Wahindu wengi wa tabaka la juu.

Mauaji ya Khan yalipelekea maelfu kuandamana katika mitaa ya India siku ya Juamtano, huku waandamanaji waitoa miito ya kukomesha wimbi hilo la vurugu za makundi chini ya kaulimbiu ya "Siyo katika jina langu".

Modi alielezea maumivu na uchungu juu ya mazingira ya sasa nchini India, akiorodhesha matukio ya vuguru za wazalendo. "Hakuna mtu katika taifa hili anaepaswa kuchukuwa sheria mikononi mwake. Vurugu hazijawahi na kamwe hazitowahi kutatua tatizo lolote," alisema waziri mkuu Modi.

Aliendelea kusimulia kuhusu kisa cha utotoni, wakati ng'ombe wa jirani alivyomburuta mtoto mchanga na kukumbuka namna mnyama huyo alivyofadhainishwa baada tukio hilo. "Hakula wala kunywa. kulikuwepo na machozi machoni mwa ng'ombe....hatimaye alifariki kwa huzuni," alisema Modi "Ng'ombe huyo alikuwa akitubu kwa vile aliumizwa na kifo cha mtoto. Lakini leo nasikia kwamba mtu anauawa katika jina la ng'ombe."

Uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu

Makundi ya haki za binadamu yameonya juu ya kujengeka utamaduni wa kinga kwa uhalifu dhidi ya Waislamu na kuitaka serikali ya Modi inayoongozw ana chama cha Kizalendo cha Wahindu kuchukuwa hatua. Mwelekeo wa uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu unaofanywa bila kuadhibiwa unatia wasiwasi mkubwa," alisema Aakar Patel, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Amnesty Interantional nchini India, katika taarifa wiki hii.

Shirika hilo la haki za binadamu limesema Waislamu wasiopungua 10 wamechomwa moto au kuuawa hadharani tangu April katika uhalifu unaoshukiwa kuwa wa chuki. Mwaka uliopita Modi aliwalaumu wazalendo na kutoa wito wa kukandamizwa kwa makundi yanayotumia dini kutenda uhalifu.

Mwanaume wa Kihindi Vijay Parsana akijipiga selfie na ng'ombe wake Poonam, aliekuwa akijianda kumuozesha na punda ajulikanaye kama Arjun, katika sherehe inayoonyesha hadhi ya ng'ombe miongoni mwa Wahindu.Picha: Getty Images/S.Panthaky

Lakini wakosoaji wanasema wazalendo wametiwa nguvu na kuchaguliwa mwaka 2014 kwa chama chake cha mrengo wa kulia cha Bharatiya Janata, na wameitaka serikali kupaza sauti zaidi katika kulaani mashambulizi hayo.

Kuchinjwa kwa ng'ombe na kumiliki au kula nyama kumepigwa marufuku katika majimbo mengi nchini India, ambapo baadhi yanaweka adhabu za vifungo vya maisha kwa ukikukaji wa sheria hiyo. Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya makundi ya kizalendo yanayolinda ng'ombe, wanaozurura katika barabara kuu wakikagua malori ya mifugo kuangalia uwepo wa mnyama huyo.

Polisi yawakamata waathirika badala ya wahalifu

Mwezi April, Mwanaume wa Kiislamu alipigwa hadi kufariki na kundi la watu katika jimbo la Rajastan baada ya kugundua ng'ombe kwenye lori lake. Mwanaume huyo alikuwa mkulima anaefuga ng'ombe wa maziwa. Mwezi uliofuata, Waislamu wawili walipigwa na kuuawa kwa madai ya kuiba ng'ombe. Katika visa vyote viwili, polisi walishutumiwa kwa kushindwa kuchukuwa hatua za haraka kuwalinda wahanga.

Katika mashamulizi ya jimbo la Rajasthan ambamo wazalendo 200 waliyavamia malori yanayosafirisha ng'ombe yakiwa barabarani, polisi ilianza kuwakamata 11 kati ya wale waliopigwa kwa madai ya kukiuka mashari ya vibali badala ya kuwakamata wakosaji.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef