1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modi amwambia Putin huu si wakati wa vita

Tafsiri: John Juma16 Septemba 2022

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amemwambia rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba huu si wakati wa vita. Hayo yamejiri pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Usbekistan Samarkand | SOC GIpfeltreffen
Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Naye rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameuambia mkutano huo kwamba anataka vita vya Ukraine kumalizika haraka iwezekanavyo. 

India na Urusi zina uhusiano wa miaka mingi tangu enzi za Vita Baridi. Hata sasa India hununua zana zake nyingi za kivita kutoka Urusi. Lakini kwenye mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kati ya viongozi wa mataifa hayo mawili, tangu Urusi kuivamia Ukraine, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alimwambia Putin kwamba anafahamu huu si wakati wa vita.

Viongozi wa SCO wasifia maendeleo ya jumuiya yao

Tangu mzozo huo uanze, India imekuwa ikichelea kuishutumu Urusi kwa uvamizi huo ambao umesababisha bei ya mafuta na bidhaa nyingine kupanda ulimwenguni.

Kwenye mkutano wao pembezoni mwa ule wa kilele unaofanyika mji wa Samarkand, Uzbekistan, wa jumuiya ya ushirikiano wa kikanda wa Shanghai SCO, Modi alisisitiza umuhimu wa demokrasia, diplomasia na mazungumzo. Kauli za Modi zimejiri siku moja tu baada ya Putin kuungama kuwa China ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi ilielezea wasiwasi wake kuhusu vita vya Ukraine.

Erdogan ahimiza vita vya Ukraine kusitishwa

Erdogan amehoji kuwa msimamo wenye usawa katika mzozo wa Ukraine unahitajika kwa sababu ya utegemezi mkubwa wa Uturuki kwa nishati kutoka UrusiPicha: Murat Kula/AA/picture alliance

Miongoni mwa wanaohuduria mkutano huo wa kilele ni rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye amekuwa akijaribu kutumia uhusiano mzuri kati ya nchi yake na Urusi kumshawishi Vladimir Putin, kufanya mazungumzo ya amani ya moja kwa moja na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky nchini Uturuki.

Katika hotuba yake Erdogan ameuambia mkutano huo kwamba nchi yake imekuwa ikifanya juhudi za kidiplomasia kuvimaliza vita vya Ukraine. Erdogan ambaye pia amefanya kikao na Putin pembezoni mwa mkutano wa SCO amesema nchi yake inataka vita vya Ukraine vimalizike haraka iwezekanavyo.

Rais Vladimir Putin ayasifia mahusiano yake na Xi Jinping

Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya Kujihami ya NATO imekuwa ikiipa Ukraine silaha, huku kwa upande mwingine ikiimarisha biashara kati yake na Urusi.

Erdogan na Modi wafanya wakutana tangu mvutano wao kuhusu Kashmir

Hapo awali Erdogan alifanya mkutano mwingine na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pembezoni mwa mkutano huo. Hiyo ilikuwa mara yao ya kwanza kukutana ana kwa ana katika miaka miwili iliyopita tangu uhusiano wao ulipoharibika kufuatia kauli za Erdogan kuhusu eneo lenye Waislamu wengi la Kashmir ambalo linazozaniwa.

Waziri Mkuu wa Narendra Modi amhimiza Vladimir Putin kuzingatia demokrasia, diplomasia na mazungumzo kumaliza vita vya Ukraine.Picha: Sergei Bobylev/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP/picture alliance

Ofisi ya Narendra Modi ilisema kupitia ukurasa wa Twitter kwamba kwenye mkutano huo, walijadili njia za kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zao katika sekta sekta mbalimbali

Mapema mwaka 2020 serikali ya India ilimuata balozi wa Uturuki nchini humo na kulalamika dhidi ya Erdogan ambaye akiwa Pakistan alisema hali ya Kashmir inazidi kuwa mbaya. Kauli yake ilijiri baada ya serikali ya Modi kuondoa utawala wa ndani wa jimbo hilo mwaka 2019 na badala yake kuliweka chini ya utawala wa serikali ya shirikisho.

Mapema Ijumaa, rais wa China Xi Jinping aliuhutubia mkutano huo na kutoa wito kwa nchi za kanda Asia kuukabili ushawishi wa madola ya magharibi duniani.

Jumuiya ya ushirikiano wa SCO iliundwa mwaka 2001 kama chombo cha kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa taasisi pinzani za Magharibi.

(RTRE, AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW