1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Modi azungumza na Putin kuhusu kukomeshwa vita vya Ukraine

Sylvia Mwehozi
27 Agosti 2024

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amemueleza Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumanne kwamba anaunga mkono kukomeshwa haraka kwa mzozo unaoendelea nchini Ukraine baada ya kuzuru nchi hiyo iliyokumbwa na vita.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: Sergei Gapon/AFP

Modi, mwenye umri wa miaka 73, amekuwa na jitihada za kudumisha uhusiano wa kihistoria wa India na Urusi huku akijenga ubia wa karibu wa kiusalama na mataifa ya Magharibi kama ngome dhidi ya mpinzani wa kikanda China. Modi amrai Zelensky kukaa mezani kumaliza vita na Urusi

India imejizuia kulaani vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022, badala yake imezitaka pande zote mbili kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo. Modi amesema kupitia ujumbe wake aliouchapisha kupitia mitandao ya kijamii kwamba "alibadilishana mitazamo juu ya mzozo wa Urusi na Ukraine" na Putin na kutoa mawazo yake kuhusu ziara yake ya hivi karibuni nchini Ukraine.

Soma: Zelensky: Nitaunga mkono India kuwa mwandaaji wa mkutano wa pili wa amani

Ameendelea kueleza kwamba "amesisitiza dhamira thabiti ya India ya kuunga mkono utatuzi wa mapema, wa kudumu na wa amani wa mzozo".

Narendra Modi wakati alipokutana na Volodymyr Zelenskiy Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Modi, ambaye aliwakasirisha Waukraine kwa kumkumbatia Putin huko Moscow hivi karibuni, alitembelea Kyiv siku ya Ijumaa na kumwambia Rais Volodymyr Zelensky kwamba "hakuna tatizo linalopaswa kutatuliwa kwenye uwanja wa vita."

Mazungumzo ya Modi na Putin yamefanyika siku moja baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Joe Biden, ambapo Modi pia ametilia mkazo "msimamo thabiti wa New Delhi katika kuegemea mazungumzo na diplomasia", kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya India.

India na Urusi zimedumisha uhusiano wa karibu tangu enzi za Vita Baridi, ambavyo vilishuhudia Kremlin kuwa msambazaji mkuu wa silaha kwa nchi hiyo ya Kusini mwa Asia. Urusi pia imekuwa muuzaji mkuu wa mafuta ghafi ya bei nafuu kwa India tangu mzozo wa Ukraine ulipoanza, hatua inayotoa fursa ya soko la nje linalohitajika baada ya kuwekewa vikwazo na nchi za Magharibi.Narendra Modi ahimiza amani kabla ya ziara ya Ukraine

Hatua hiyo imerekebisha kwa kiasi kikubwa uhusiano wao wa kiuchumi na kuzinufaisha nchi zote mbili. India ni sehemu ya kundi la nchi za Quad, pamoja na Marekani, Japan na Australia, ambazo zinajizatiti dhidi ya ushawishi unaoongezeka wa China katika eneo la Asia-Pasifiki.