1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modi asaini mikataba minane na Kagame

Slyvanus Karamera24 Julai 2018

Rwanda na India zimetiliana saini mkataba wa dola milioni 400 mjini Kigali, ambazo zitaisaidia Rwanda katika sekta mbalimbali za maendeleo. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi yupo nchini humo kwa ziara ya siku mbili.

Ruanda PK Präsident Paul Kagame mit indischem Ministerpräsidenten Narendra Modi
Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

Waziri Mkuu wa India aliwasili jijini Kigali Jumatatu jioni akiwa na ujumbe mkubwa wa wawekezaji na mawaziri kadhaa katika serikali yake. Waziri mkuu huyo alikutana kwa mazungumzo na mwenyeji Rais Paul Kagame wa Rwanda katika mazungumzo wakiwa wawili na baadaye wakafanya mazungumzo wakiwa pamoja na ujumbe wa pande mbili.

Baadaye viongozi hao waliongoza zoezi la kutia saini mikataba minane ambayo ilisainiwa na mawaziri au viongozi husika kutoka kila upande.

Kwenye mikataba hiyo minane, mmoja una thamani ya milioni 400 na unahusu ujenzi wa kanda maalum za viwanda vya kisasa likiwemo eneo maalum la viwanda lililoko nje kidogo ya mji mkuu, Kigali.

Mkataba mwingine wa thamani ya dola za Marekani milioni 200 unahusu kuinua sekta ya kilimo hasa cha umwagiliaji.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, amesema kwamba nchi yake inafanya hivyo kutokana na utendaji kazi wa serikali ya Rwanda ambayo ameitaja kama inayozingatia kanuni za uongozi bora kama mapambano ya ulaji rushwa na kufanya kazi kwa uwazi.

"Baada ya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii wa watutsi wa Rwanda, amani,utulivu na maendeleo yanayoshuhudiwa ktk nchi hii ni ishara kwamba serikali ya nchi hii inafanya mambo kwa umakini mkubwa.Nchi hii ina kasi kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na sisi kama serikali ya India tunasema ni lazima tushirikiane na nchi yenye hali kama hii katika mkakati wake wa maendeleo," amesema Modi.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiwasili mjini Kigali, RwandaPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Ng'ombe 200 kwa famili za Rwanda

Mikataba mingine iliyotiwa saini na serikali za nchi hizo mbili inahusu ushirikiano wa ulinzi na usalama, biashara, utamaduni na sayansi na teknolojia. Baadhi ya mikataba hii ni misaada na mikopo yenye riba na masharti nafuu.

Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Uumoja wa Afrika, amesema kwamba pamoja na mikataba hiyo, yeye na waziri mkuu wa India wamezungumzia pia masuala mbalimbali yanayohusu kanda ya Maziwa Makuu, bara la Afrika na hata diplomasia na siasa zinazoendelea ulimwenguni.

"Mimi na waziri mkuu tumezungumza kinaugaubaga kuhusu ushirikiano wa nchi mbili pamoja na bara la Afrika, lakini hata mambo mengine yanayoendelea ulimwenguni. Ziara hii ya kihistoria ya waziri mkuu wa India nchini Rwanda ni ishara ya uhusiano wa kihistoria baina ya mataifa yetu. Nchi zetu zina sera sawa ya kuhakikisha tunawasaidia wananchi wetu kupata maendeleo endelevu," amesema Kagame.

Mapema asubuhi ya  Jumanne, Modi alitembelea jumba la makumbusho ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi na Wahutu lililoko mjini Kigali. Baadae akaelekea wilaya ya mashariki ambako ametoa msaada wa ng'ombe mia mbili kwa familia zisizojiweza, ili kusaidia mpango wa serikali ya Rwanda unaojulikana kama: "Ng'ombe mmoja kwa familia maskini."

Waziri mkuu wa India atakamilisha ziara yake nchini Rwanda jioni ya Jumanne na kuondoka kuelekea Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa kilele wa mataifa matano yanayoinukia kwa kasi kiuchumi, BRICS, unaoanza Jumatano.

Mwandishi: Sylvanus Karemera/DW Kigali

Mhariri: Mohammed Khelef