1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Modi ziarani nchini Ukraine kwa mazungumzo na Zelensky

23 Agosti 2024

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi yuko Ukraine kwa mazungumzo na Rais Volodymyr Zelensky.

India Ukraine | Narendra Modi ziarani Kyiv
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi (kushoto) akilakiwa na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine mjini Kyiv. Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Modi aliwasili mjini Kyiv mapema leo asubuhi na kulakiwa na maafisa wa Ukraine kwenye kituo kikuu cha treni akitokea Poland kabla ya kuelekea kwenye mazungumzo na Rais Zelensky.

Mchana huu alikaribishwa na Zelensky kwenye ikulu ya nchi hiyo tayari kuanza mazungumzo ambayo maafisa wa pande zote mbili wanasema yatajikita katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, ulinzi na teknolojia.

Lakini wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema India inalenga kuitumia ziara hiyo kudhihirisha msimamo wake iliyoutangaza tangu kuanza kwa vita kwamba haitochagua upande.

Mkuu wa utumishi wa ikulu ya Ukraine Andriy Yermak ameitaja ziara ya Modi -- ambayo ni kwanza kufanya na kiongozi wa India tangu Ukraine ilipotangaza uhuru kutoka Dola ya Kisovieti mwaka 1991 -- kuwa ya "kihistoria".

Amesema Ukraine ina matumaini kwamba India itakuwa na dhima katika kumaliza vita baina ya nchi yake na Urusi chini ya misingi ya haki.

Modi anaitembelea Kyiv baada ya ziara ya Moscow iliyozusha ukosoaji 

Safari ya Modi mjini Kyiv inafanyika kiasi mwezi mmoja tangu alipomtembelea Rais Vladimir Putin mjini Moscow kwa ziara iliyokosolewa sana na viongozi kadhaa wa mataifa ya magharibi.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alipokutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mwezi Julai mjini Moscow. Picha: Sergei Bobylev/POOL/TASS/picture alliance/dpa

Wengi waliuona uamuzi huo wa Modi kuwa ishara ya India kujiegemeza zaidi na Urusi ambayo usuhuba kati yao umeimarika tangu kuanza kwa vita.

India inajipatia mafuta kwa bei chee kutoka Urusi pamoja na teknolojia ya silaha na vipuri vya kijeshi.

Wakati wa ziara hiyo ya mwezi Julai, rais Zelensky wa Ukraine alisema bila woga kwamba safari ya Modi mjini Moscow ilikuwa "pigo kubwa kwa juhudi za kutafuta amani". Vilevile alimkosoa kiongozi huyo kwa kumkumbatia Putin wakati wa mkutano wao.

Ziara ya Modi mjini Kyiv hivi leo inafanyika siku moja kabla ya Ukraine kusherehea siku ya uhuru iliyoutangaza Agosti 24 mwaka 1991 kutoka iliyokuwa dola kubwa ya Muungano wa Kisovieti.

Mapema leo asubuhi Zelensky alishiriki tukio la kupandisha bendera ya taifa na kuzungumza na wanajeshi wa nchi yake kuhusu umuhimu wa kushinda vita na Urusi.

"Katika vita hivi tunapigania haki ya Ukraine na raia wake. Haki kwa kile kilicho cha kwetu. Haki kwa uhuru wetu, kwa heshima ya taifa letu na usalama wetu." alisema Zelensky. 

Moscow yasema Ukraine ilijaribu kukishambulia kinu cha nyuklia huko Kursk 

Mashambulizi ya Ukraine kwenye mkoa wa Urusi wa Kursk. Picha: 95th Air Assault Brigade/via REUTERS

Wakati yote hayo yakiendelea, Urusi na Ukraine zimeendelea kupambana kwenye uwanja wa vita. Hii leo Moscow imeituhumu Ukraine kujaribu kukishambulia kinu cha nyuklia kwenye mkoa wa Kursk ambao vikosi vya Ukraine viliuvamia mwanzoni mwa mwezi huu.

Urusi imelitaja jaribio hilo kuwa "ugaidi wa nyuklia". Ukraine haijasema chochote juu ya tuhuma hizo. 

Katika hatua nyingine moto uliozuka kwenye bandari ya Uursi ya Kavkaz inayosambaza bidhaa kwenye rasi ya Crimea bado unawaka siku moja tangu kivuko kilichosheheni matangi ya mafuta kuzama kutokana na shambulizi la droni la Ukraine.

Jeshi la wanamaji la Ukraine lilikiri kukizamisha kivuko hicho inachosema kilikuwa kinatumika kupeleka silaha na mafuta kwenye rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mwaka 2014.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW