Moenchengladbach yaifukuzia Dortmund kileleni mwa Bundesliga
22 Oktoba 2018Jonas Hofmann alipachika mabao matatu jana ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuanza kucheza kandanda katika ngazi ya juu jana, wakati Borussia Moenchengladbach ilipojiweka katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi katika Bundesliga kwa kuizaba Mainz 04 kwa mabao 4-0.
Baada ya ushindi wa kushangaza wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa watetezi Bayern Munich wiki tatu zilizopita, ushindu huu ni ishara kubwa kutoka kwa kocha Dieter Hecking na kikosi chake, ambaye aliiweka timu hiyo katika nafasi ya pili nyuma ya Borussia Dortmund ambao wanashikilia nafasi hiyo baada ya Jumamosi kuikandika VFB Stuttgart kwa mabao 4-0 pia.
Ushindi wa Gladbach umeiacha Bayern Munich mabingwa watetezi katika Bundesliga katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 16.
Borussia Dortmund
Vinara wa ligi hiyo hivi sasa ni Borussia Dortmund ambayo ina pointi 20, ikifuatiwa na Borussia Moenchengladbach yenye pointi 17 sawa na Werder Bremen timu ambayo iliididimiza makamu bingwa wa Bundesliga Schalke 04 katika mzozo mkubwa baada ya kuitandika kwa mabao 2-0 nyumbani siku ya Jumamosi jioni.
Schalke 04 iko nafasi ya 16 ikiwa na pointi 6 tu kibindoni. Nafasi ya Schalke kuwania kucheza katika mashindano ya Ulaya Champions League ama Europa League imo mashakani mara hii, kutokana na umbali uliopo kati yake na timu zilizoko juu.
Bayern Munich imesafiri kwenda Ugiriki kukabiliana na AEK Athens katika Champions League kesho Jumatatu ikiimarishwa na ushindi katika Bundesliga ambao ni kama ukombozi baada ya kupata matokeo mabaya, katika uchezaji. Mbinyo ulikuwa ukizidi kwa mabingwa hao wa Ujerumani pamoja na kocha wao mpya Niko Kovac kutokana na kutoshinda katika michezo minne na kusababisha viongozi wa juu wa klabu hiyo ikiwa ni pamoja na Karl-Heinz Rummenigge na Uli Hoeness kushambulia vyombo vya habari.
Lakini ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Wolfsburg katika Bundesliga , ambamo Robert Lewandowski alipachika mabao mawili na kufikisha mwisho ukame wa magoli katika michezo minne, unasifiwa kama sehemu muhimu ya mabadiliko ya majaaliwa ya Bayern Munich msimu huu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman