1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moenchengladbach yasonga nafasi ya nne

4 Aprili 2016

Borussia Moenchengladbach imepanda katika nafasi za kucheza kandanda la Champions League, baada ya kuiduwaza Hertha Berlin 5-0

Fußball Bundesliga Borussia Moenchengladbach gegen Hertha BSC
Picha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Gladbach iliicharaza Hertha 4-1 mjini Berlin mwezi Oktoba na tena ilikuwa moto wa kuotea mbali uwanjani Borussia Park jana huku Thorgan Hazard akifunga mbili, na Patrick Hermann na Ibrahima Traore wakifunga moja kila mmoja.

Gladbach hivyo imesonga kutoka nafasi ya saba hadi ya nne na sasa iko nyuma ya Hertha na pengo la pointi tatu tu. Andre Hahn ni kiungo wa Galdbach "Adui kawaida huwa bora zaidi ikiwa utamruhusu, na leo tumekuwa na mchezo mzuri sana. Tumehimili mapambano, tumefanya kazi nzuri kama timu na tukawazuia Hertha kutamba. Bila shaka tulijua Berlin ni wagumu".

Hoffenheim iliponea nafasi za kushushwa daraja kwa kutoka sare ya 1-1 nyumbani kwa Cologne. Siku ya Jumamosi, Franck Ribery alirejea katika kikosi cha Bayern katika njia ya kipekee kwa kuifungia goli safi sana la ushindi wa 1-0 dhidi yanambari mbili kutoka mkia Eintracht Frankfurt.

Borussia Dortmund ina uhakika wa Champions LeaguePicha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Ikiwa imesalia mechi sita tu, vijana hao wa Pep Guardiola, ambao wanaongoza kwa pengo la pointi tano, wanalenga kuwa timu ya kwanza ya Ujerumani kushinda mataji manne mfululizo ya Bundesliga.

Nambari mbili Borussia Dortmund ilitoka nyuma na kushinda 3-2 dhidi ya Werder Bremen ushindi uliowapa kibali cha moja kwa moja cha kucheza Champions League msimu ujao. Marcel Schmelzer ni beki wa Dortmund "Nna furaha sana kwamba sisi kama timu, tumefaulu kupiga kona pamoja na matumaini tuliyo nayo kwa sasa. Ukweli ni kuwa wachezaji wengine wameingia kikosini na kuleta matokeo muhimu, na tuna furaha kwa ajili ya wachezaji hawa wawili: Shinji na Adrian ambacho ni kitu kizuri na kinahimiza ari ya timu tuliyo nayo kikosini".

Augsburg imesalia katika nafasi ya 16 baada ya kubamizwa 4-2 dhidi ya Mainz. Washika mkia Hanover 96 walimfungasha virago kocha mkuu Thomas Schaaf hapo jana baada ya kuzabwa 3-0 na Hamburg, kichapo chake cha kumi katika mechi 11. Schalke ilidondoka katika nafasi ya saba, na inakabiliwa na hatari ya kukosa kibali cha Europa League msimu ujao, baada ya kunyoroshwa 3-0 na Ingolstadt. Darmstadt iliondoa katika kinyang'anyiro cha kushushwa ngazi baada ya sare ya 2-2 na Stuttgart.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu