1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogadishu yapiga kura ya moja kwa moja ya serikali za mitaa

25 Desemba 2025

Mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, unaendesha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa Alhamisi ukiwa wa kwanza wa upigaji kura ya moja kwa moja kwa wananchi wote katika muda wa karibu miaka 60.

Somalia Mogadischu 2025 | Wapiga kura washiriki kwenye zoezi la kupiga kura
Zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa jijini Mogadishu mwaka 2025Picha: Hassan Ali Elmi/AFP

Ulinzi mkali umewekwa pamoja na jiji kufungwa kabisa. Uchaguzi huu unafanyika wakati taifa hilo likijaribu kujinasua kutoka kwenye miongo ya migogoro, likikabiliana na uasi wa wanamgambo wa Al-Shabaab na pia majanga ya asili ya mara kwa mara.

Zoezi hilo linatajwa kama jaribio la mfumo wa upigaji kura wa moja kwa moja unaoungwa mkono na Rais Hassan Sheikh Mohamud, ingawa limekumbwa na upinzani kutoka kwa majimbo, wanachama na vyama vikuu vya upinzani ambavyo vimeususia uchaguzi.

Takribani wagombea 1,600 wanashindania viti 390 vya halmashauri katika eneo la Banadir, huku wapiga kura wapatao 400,000 wakitarajiwa kushiriki.

Kwa mujibu wa mamlaka za uchaguzi, usafiri wote utasimamishwa siku ya kura, uwanja mkuu wa ndege utafungwa, na zaidi ya maafisa 10,000 wa usalama watapelekwa kulinda zoezi hilo.

Uchaguzi huu unatajwa kuwa wa kihistoria, lakini wachambuzi wanaonya kuwa mvutano wa kisiasa na hali ya usalama vinaweza kuathiri mustakabali wa demokrasia nchini Somalia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW