MOGADISHU:Mshukiwa wa Al Qaeda auawa Somalia
10 Januari 2007Mshukiwa wa ngazi za juu wa kundi la Al Qaeda anayesakwa na Marekani kwa kuhusika na shambulio la bomu katika balozi za nchi hiyo nchini Kenya na Tanzania mwkaa 98 ameuawa.Hayo ni kwa mujibu wa afisa wa serikali ya Somalia huku mashambulio ya Marekani ya ndege yakiendelea kwa siku ya tatu nchini Somalia. Kifo cha mshukiwa huyo Fazul Abdullah Mohammed kilielezwa kwa kirefu katika taarifa ya ujasusi ya Marekani iliyowasilishwa kwa serikali ya Somalia.
Mohammed ni mmoja wa watu wanaosakwa na shirika la ujasusi la marekani FBI aliyekwepa kukamatwa kwa miaka minane anadaiwa kuwa alipewa hifadhi na wapiganaji wa kiislamu wanaochagiza majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na majeshi ya Ethiopia.
Wakati huohuo naibu waziri mkuu wa Somalia anasema kuwa majeshi ya marekani yanahitajika ili kuwafurusha wapiganaji walio na msimamo mkali nchini mwake na kwamba anataraji majeshi hayo yatawasili hivi karibuni.
Yapata ndege nne aina ya AC 130 zimeripotiwa kushambulia eneo la Ras Kamboni lililo katika pwani ya Somalia kilomita chache kutoka mpaka wa Kenya.Eneo hilo lilishambuliwa mwanzoni mwa juma na ndege za Marekani.
Marekani kwa upande wake inapinga kuhusika na mashambulio mawili yaliyotokea baadaye katika eneo hilo yaliyoripotiwa na Wizara ya Ulinzi ya Somalia.
Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kwa pamoja walishtumu mashambulio hayo.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon anaonya kuwa huenda matukio hayo yakachochea uhasama katika eneo hilo.Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linakutana ili kujadilia mapendekezo ya kupeleka kikosi cha kulinda amani nchini Somalia.