Mohammed Mursi kufunguliwa mashitaka Misri
26 Julai 2013Jaji aneyesimamia kesi inayochunguza kuhusika kwa Mursi na kundi la Hamas la Palestina linalodaiwa kumsaidia kiongozi huyo kutoroka jela mwaka 2011 ametoa agizo hilo hii leo la kutaka Mursi azuiliwe.
Shirika la habari la serikali MENA limeripoti kuwa kifungo hicho kinaweza kuongezwa huku uchunguzi ukiendelea na kuwa tayari Mursi ameshahojiwa.
Msemaji wa udugu wa kiislamu Gehad El Haddad amesema agizo hilo la mahakama la kumzuilia Mursi linaashiria kuwa utawala wa kiimla uliopita umerejea kwa kishindo madarakani.
Kesi hiyo inahusisha kutoroka gerezani kwa viongozi kadhaa wa udugu wa kiisalmu wakati wa harakati zilizomuondowa madarakani Mubarak mwaka 2011.Kumekuwa na ripoti kadha wa kadha katika vyombo vya habari vya Misri kuwa udugu wa kiislamu ulishirikiana na Hamas na wanamgambo wa Hezbollah kutoka Lebanon katika kisa hicho cha kutoroka jela.
Maafisa wa udugu wa kiislamu wamekuwa wakisema walisaidiwa na raia wa Misri na wala si watu wa kutoka nje ya nchi hiyo.Jeshi la Misri limekuwa likimzuilia Mursi tangu tarehe 3 mwezi huu katika eneo lisilojulikana.
Mursi anachunguzwa kwa mashitaka chungunzima
Shirika la habari la MENA limeripoti kuwa Mursi anachunguzwa kwa madai ya kushirikiana na Hamas katika vitendo dhidi ya serikali,kushambulia vituo vya polisi,wanajeshi na magereza na kuwasaidia wafungwa kutoroka akiwemo yeye mwenyewe na kuua maafisa wa serikali wanjeshi na wafungwa kwa kukusudia.
Tangazo hilo linakuja baada ya mkuu wa jeshi la Misri Jenerali Abdel Fattah al Sisi kuitisha maandamano makubwa leo ili kulipa jeshi hilo mamlaka ya kukabilina na kile alichokiita ugaidi na ghasia zilizoikumba nchi hiyo tangu kung'olewa kwa Mursi wiki tatu zilizopita.
Udugu wa kiislamu pia umeitisha maandamano leo na kuzua hofu ya kutokea makabiliano makali kati ya makundi hayo mawili ya waandamanaji.
Afisa mmoja wa jeshi amesema jeshi limetowa muda wa hadi kesho Jumamosi kundi la Udugu wa kiislamu likomesha uasi na kujiunga katika mchakato wa kisiasa uliowekwa na jeshi utakaoandaa chaguzi.
Hofu kuhusu ukandamizaji wa udugu wa kiislamu
Kundi la udugu wa kiislamu linahofia kumezuka ukandamizaji wa kuondolea mbali vuguvugu hilo la kiislamu ambalo liliibuka baada ya miongo mingi ya kukandamizwa na kushinda katika uchaguzi baada ya kung'olewa madarakani Hosni Mubarak na sasa mwaka mmoja baadaye nao wamepinduliwa na jeshi.
Hali hiyo ya msukosuko imezua wasiwasi katika mataifa ya magharibi.Marekani imeahirisha kutuma ndege za kijeshi nchini humo na kulitaka jeshi la Misri linalopokea msaada wa dola bilioni 1.5 kila mwaka kujizuia na kuchukua kila tahadhari katika maandamano ya leo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametaka kuachiliwa huru kwa Mursi na washirika wake au kesi zao zishughulikiwe kwa uwazi na bila kucheleweshwa.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap
Mhariri :Yusuf Saumu