Moise Katumbi azuiwa kurejea Congo
4 Agosti 2018Kiongozi huyo wa upinzani alizuiwa kurejea nyumbani ameahidi kupambana ili kufanyika uchaguzi halisi.
Moise Katumbi , mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga , alizuiliwa kuingia katika jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kushitakiwa kwa makosa dhidi ya usalama wa taifa, maafisa wamesema. Katumbi mwenye umri wa miaka 53, amekuwa akiishi uhamishoni alikomua binafsi nchini Ubelgiji tangu Mei 2016 baada ya kutofautiana na rais Joseph Kabila, ambaye ameitawala DRC kwa miaka 17.
Alipanga kurejea nchini humo kwa ndege ya binafsi kutoka Johannesburg kwenda Lubumbashi, mji mkuu wa jimbo la Katanga, kuwasilisha fomu zake za kuwania urais katika uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu mwezi Desemba, hatua ambayo itaongeza mbinyo kwa rais Kabila.
Lakini meya wa mji wa Lubumbushi alimkatalia ruhusa ya kuingia, wakati ofisi ya mwendesha mashitaka imesema Katumbi ameshitakiwa kwa "kuhatarisha usalama wa ndani ya nje" na atakamatwa iwapo atarejea. Mwandishi habari wa redio ya Ufaransa RFI amesema Katumbi badala yake aliwasili katika mpaka wa Zambia na DRC wa Kasumbalesa.
Vidio zilizowekwa katika mtandao na wasaidizi wake pamoja na watu wengine zinamuonesha akiwa katika upande wa mpaka wa Zambia, akisalimiana na mamia ya waungaji wake mkono katika gari yake.
"Serikali inanizuwia kutua na inafunga mpaka, uhalifu wangu? Kutaka kuingia nchini mwangu na kuwasilisha fomu za kuomba urais," Katumbi aliandika katika ukurasa wa Twitter.
"Kwa kujaribu kunizuwia, wanataka kuwanyima Wakongo haki yao ya uchaguzi halisi. Nitapambana," ameongeza.
Mashitaka dhidi ya Katumbi
Katika upande wa mpaka wa Congo , majeshi ya usalama yamechukua hatua dhidi ya waandamanaji ambao walikuwa wakirusha mawe hewabi, polisi ya Congo imesema , na kuongeza kwamba dereva wa lori la Tanzania amejeruhiwa kidogo. Takriban vituo viwili vya polisi vya upekuzi viliwekwa ili kufanya upekuzi hadi katika uwanja wa ndege wa Lubumbashi jana Ijumaa na barabara kuu ya mji huo kwenda Zambia ilifungwa kwa kutumia lori, mwandishi habari wa shirika la habari la afp alisema.
Katumbi anatakabiliwa na kukamatwa baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela wakati akiwa hayupo mahakamani mwezi Juni 2016 katika kesi ya madai ya udanganyifu wa mali. Pia anashutumiwa kwa kukodi mamluki na kuwa na pasi ya kusafiria ya italia, ambapo sheria za Congo haziruhusu mtu kuwa na uraia pacha wa mataifa mawili. Anakana madai hayo yote katika kesi hizo mbili.
Hasimu mwingine wa Kabila , mbabe wa zamani wa kivita na makamu wa zamani wa rais Jean-Pierre Bemba , mwenye umri wa miaka 55 , alirejea nyumbani wiki hii. Amewasilisha rasmi ombi lake la kuwania urais siku ya Alhamis.
DRC haijawahi kufanya mabadiliko ya amani ya uongozi tangu ilipopata uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960, na baadhi ya wataalamu wanahofia kwamba uchaguzi wa Desemba 23 huenda ukazusha mzozo mwingine utakaomwaga damu.
Kabila mwenye umri wa miaka 47 , amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, akiliongoza taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini na ambalo linasifika kwa rushwa, kutokuwa na usawa na machafuko.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isacc Gamba