Moldova: Rais Sandu ashinda uchaguzi wa urais uliorudiwa
4 Novemba 2024Rais wa sasa wa Moldova Maia Sandu, amesema ameshinda katika duru ya pili ya uchaguzi wa siku ya Jumapili. Matokeo ya kura hiyo yanaweza kuwa na jukumu muhimu katika mustakabali wa nchi hiyo katika bara la Ulaya.
Uchaguzi huo vilevile ulikabiliwa na hofu ya kuingiliwa kati na Urusi.
Sandu anayeunga mkono Umoja wa Ulaya alikabiliana na mwendesha mashtaka mkuu wa zamani Alexandr Stoianoglo, ambaye aliungwa mkono na Chama cha Kisoshalisti kinachoiunga mkono Urusi, katika kura ya pili iliyokuwa na ushindani mkali.
Rais Maia Sandu alikuwa na asilimia 54.7 ya kura,bada ya karibu asilimia 99 ya kura zote kuhesabiwa kulingana na mamlaka ya uchaguzi ya Moldova. Mgombea mwingine Alexandr Stoianoglo, alikuwa amepata asilimia 45.3 ya kura katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi.
Soma Pia: Moldova yapiga kura katika uchaguzi tete kuhusu mustakabali wa EU
Kwa wananchi wengi wa Moldova, Rais Maia Sandu, amekuwa ishara ya mabadiliko katika nchi hiyo iliyokuwa zamani katika jamhuri ya kisovieti wakati anapojaribu kulielekeza taifa hilo kwenye njia mpya ya kujiunga na Umoja na Ulaya.
Kiongozi huyo wa Moldova Maia Sandu mwenye umri wa miaka 52 aliomba nchi yake ijiunge na jumuiya ya Umoja wa ulaya mnamo mwaka 2022, amepitisha mageuzi mapananchini mwake kwa ajili ya kupambana na ufisadi na ameweza kuvutia kuleta uwekezaji.
Viongozi kadhaa wa Ulaya wamempongeza Sandu kwa ushindi wake wakiwemo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ambaye amesema Sandu ameiongoza Jamhuri ya Moldova kwa usalama katika nyakati ngumu na kameiweka nchi yake hiyo kwenye njia ya kuelekea kuwa Pamoja na bara Ulaya. Scholz amesema Ulaya itasimama upande mmoja na Moldova.
Vyanzo: RTRE/AFP/DPA/AP