Mombasa: Visa vya kulawiti watoto vyaongezeka
22 Oktoba 2019Ripoti zinaonyesha kwa siku za hivi karibuni visa hivyo vimeongezeka na wanaowalawiti watoto ni majirani, watu katika familia na wazazi wa kiume.
Kulingana na muuguzi mshauri katika kituo cha kushughulikia wahanga wa dhulma za kingono katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani ya Kenya - Makadara, Saida Mwinyi, watoto wanaolawitiwa ni wa kike na wa kiume na visa hivyo vinaripotiwa kwa wingi katika majimbo ya Kisauni na Nyali.
"Kwa mwezi mmoja watoto wapatao hamsini wanadhulumiwa kingono katika majimbo hayo ya bunge, huku sita yakiwa katika kaunti ya Mombasa," anasema Saida Mwinyi.
Muhimu ni kutunza bikra!
Inaripotiwa kuwa baadhi ya jamii zinazothamini ubikira, wanapofahamu mtoto wao wa kike amelawitiwa huwa hawalichukulii jambo hilo kwa uzito kwa kufahamu kwamba ubikira wake haujaharibika.
Kiasi cha robo tatu cha wanaodhulumiwa kimapenzi wanafika katika kituo hicho baada ya siku tatu jambo ambalo linawafanya kutopata matibabu ya kuzuia mimba na magonjwa ya zinaa.
Wakili Elizabeth Aroka anasema sheria inamlinda mtoto dhidi ya ubakaji, unajisi na ulawiti na kwamba anayepatikana na kosa hilo kwa mtoto wa chini ya umri wa miaka kumi na moja kifungo chake ni maisha na kwa mtoto wa umri baina ya miaka kumi na mbili hadi kumi na nne kifungo cha chini ni miaka ishirini na akiwa na umri wa miaka 16 hadi 18 kifungo cha chini ni miaka kumi na tano.
Kulingana na shirika la masuala ya haki za kiuzazi la ICRH idadi kubwa ya waathiriwa wa kingono hawapati haki zao za kisheria kwa sababu ya kukosa ufahamu wa njia zipi za awali za dharura zinazofaa kuchukuliwa baada ya kulawitiwa.
Mandishi: Faiz Abdallah Musa