1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mombasa: Washukiwa wa mihadarati wahukumiwa miaka 30 jela

Eric Ponda1 Novemba 2018

Mahakama ya Mombasa imewakuta washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati na hatia na kuwahukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Kenia Urteil im Prozess um Heroinhandel
Picha: DW/E. Ponda

Mahakama kuu mjini Mombasa imewahukumu jumla ya kifungo cha miaka 30 gerezani washtakiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati kwenye kesi ya ulanguzi ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka mtatu sasa. Hukumu hiyo sasa inafikisha kikomo sakata ya ulanguzi huo wa mihadarati, iliyonaswa kwenye Meli ya kifahari ya Baby Iris na ambayo hatimaye iliyoteketezwa mwaka wa 2015 na Serikali ya Kenya kwenye Bahari Hindi mjini humo, ikiwa na Mihadarati aina ya Heroin ya thamani ya shilingi milioni 28 pesa za Kenya.

Jaji Julius Nang'ea aliwatia hatiani washtakiwa hao wawili Ahmed Said Bakari na mwenzake Clement Serge Bristol raia wa Uhselisheli kuwa wahusika wakuu kwenye shtaka hilo la Uanguzi wa mihadarati iliyopatiiana ndani ya meli hiyo katika pwani ya Mji wa Kilifi miaka mitatu iliyopita.

Hivyo Ahmed Said Bakari alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani na faini ya shilingi milioni 13 pesa za Kenya au ahudumu mwaka mmoja Zaidi Gerezani.

Mihadarati ilikutikana ndani ya meli ndogo Kilifi Kenya

Kwa upande wake Clement Serge Briston ambaye ndiye alikuwa nahodha wa meli hiyo alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani kwa hatia ya kupatikana na dawa hizo ndani ya chombo chake, na kifungo kingine cha miaka mitano kwa kosa la kuwa na nia ya kuzisafirisha dawa hizo hadi nchini Madagascar.

Jaji Nang'ea pia alimtoza faini ya shilingi milioni 5 au kuhudumu kifungo cha mwaka mmoja Zaidi gerezani kwa kuendesha biashara hiyo ndani ya ardhi ya Kenya kinyume cha sheria.

Washtakiwa wengine watatu waliachiliwa baada ya kubainika kwamba walikuwa abiria tu kwenye chombo hicho.

Chombo hicho kilikamatwa katika Pwani ya Kilifi mnamo mwaka wa 2015 na ikiwa na mihadarati hiyo na kasha baadaye kuteketezwa katika bahari hindi chini ya uangalizi wa jeshi la Wanamaji nchini Kenya na kushuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta. Meli hiyo ya Baby Iris, kutoka Singapore ilikuwa ikiwasafirisha watalii kutoka pwani ya Kenya hadi Nchini Tanzania na Madagascar.

Kesi dhidi ya ndugu wa familia ya Akasha

Vita dhidi ya mihadarati nchini Kenya hususan Mji wa Mombasa vilipamba moto na kupelekea kukamatwa kwa Ndugu wawili Baktash Akasha na Ibrahim Akasha mwaka uliopita na kusafirishwa hadi nchini Marekani ambako wamekiri mashtaka sita ya Ulanguzi wa mihadarati.

Licha ya Mawakili wa washtakiwa hao kupinga hatua hiyo hiyo wakidai kwamba Mahakama ya Marekani haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Ndugu hao wawili sasa wanasubiri uamuzi wa mahakama hiyo ya Mji wa New York baada ya kushangaza ulimwengu kwa kukiri makosa hayo sita.

Familia ya Akasha ndiyo inayotuhumiwa kwa kuendesha mtandao wa biashara yta ulanguzi wa mihadarati kati ya Mji wa Bandari wa Mombasa na masoko ya Kigeni.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW