Monaco ina kibarua kigumu dhidi ya Juve
9 Mei 2017Monaco pamoja na Atletico Madrid zinakabiliwa na majukumu ambayo yanaonekana kuwa karibu ya kutowezekana katikati ya wiki hii katika michezo ya mkondo wa pili wa nusu fainali ya kombe la ligi ya mabingwa , Champions League barani Ulaya, ambapo wapinzani wao Juventus na Real Madrid wapo katika ukingo wa kukutana mjini Cardiff katika fainali ya mwaka huu 2017.
Hata kocha wa Monaco Leonardo Jardim anaukadiria mchezo huo kwa kiwango cha nafasi moja tu katika 20 zilizopo. Na wengi wangesema kwamba huo ni msimamo wa matumaini kwa nafasi ilizonazo kikosi chache chenye wachezaji wachanga kuweza kubadilisha matokeo ya awali ya mabao 2-0 dhidi ya Juventus Turin.
Mabingwa hao watarajiwa wa ligi ya Ufaransa ambao hupachika mabao bila shida katika ligi ya nyumbani , wamepachika mabao 3 mara 27 msimu huu. Lakini hakuna timu iliyokwisha fanya hivyo dhidi ya ngome ya Juventus ambayo imeruhusu mabo mawili , mara tano tu katika michezo 51 katika kampeni ya mwaka huu, haijashindwa nyumbani katika muda wa miezi 20 na ngome yake imevujisha mabao mawili tu katika michezo 11 ya Champions League.
Takwimu hizi zinatoa nguvu zaidi kwa Bibi Kizee, wakati timu hiyo ikiwa na uwezo wake wote wa wachezaji, kama ilivyokuwa wakati walipofanikiwa kutuliza mzuka wa washambuliaji hatari wa Monaco katika mji wa kitalii wa Monaco wiki iliyopita, ama wakati Leo Messi na wenzake wa Barcelona walipopigwa sindano ya ganzi na kuendeshwa mchakamchaka mjini Turin.
Kutokana na hilo, kocha wa Monaco Jardim alisema jukumu lake la kwanza lilikuwa kuingiza imani katika kikosi chake kwamba hawapambani na dude lililokufa.
"ni wajibu wetu kufanya kitu tofauti. Iwapo unashindwa nyumbani kwa mabao 2-0 ni wazi kwamba unapaswa kuja na kitu cha ziada," Jardim alisema katika mkesha wa kuamkia mchezo huo.
"Mjini Monaco tulipata kipigo kutokana na uzoefu: mikwaju yetu kuelekea golini ilikuwa sawa na Juventus. Tofauti ilikuwa kiwango cha mafanikio yao kilikuwa asilimia 100, kwa upande wetu ilikuwa ziro." Ameongeza Jardim.
Kocha wa Juve Massimiliano Allegri alicheka baada ya kuambiwa kwamba matokeo yamekamilika na timu yake tayari ni mshindi. "Huwezi kujua kile kitakachotokea katika mchezo. Monaco huenda wakaingia katika mchezo huo katika mtindo tofauti kabisa na kufanya hali kuwa ngumu na wana wachezaji wenye uwezo mkubwa, vipaji vya juu kabisa," amesema.
"Tunapaswa kuanza mwanzo kabisa , tuhakikishe tunacheza kwa nguvu katika mchezo huo na matumaini ni kwamba tutakuwa bora kiufundi kuliko tulivyokuwa kule Monaco, ambako tulipata fursa nyingi na kutengeneza mazingira yaliyoleta hatari na mara nyingi tulifanya makosa.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga