1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mondlane atishia kuanzisha vurugu kubwa Msumbiji

17 Desemba 2024

Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane aitaka mahakama ya juu kujizuia kuyathibitisha matokeo ya urais yaliyompa ushindi Daniel Chapo la sivyo ataanzisha vurugu kubwa Msumbiji kuanzia Jumatatu.

Maandamano mjini Maputo
Maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguziPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Msumbiji,anayedai kuwa mshindi halali wa uchaguzi uliopita, ametishia kuzusha vurugu nchi nzima, ikiwa mahakama ya juu nchini humo itaamuwa kuidhinisha ushindi wa Daniel Chapo.

Uchaguzi wa rais nchini Msumbiji, ulimalizika tangu Oktoba 9 na matokeo yalimpa ushindi mgombea wa chama tawala cha Frelimo Daniel Chapo mwenye umri wa miaka 47.

Daniel Chapo Picha: AP/dpa/picture alliance

Lakini hadi sasa nchi hiyo imekuwa ikishuhudia maandamano yanayoongozwa na kiongozi wa upinzani  Venâncio Mondlane,anadai Chapo ametangazwa mshindi na tume lakini yeye ndiye mshindi halali aliyechaguliwa na wananchi wa Msumbiji.

Mahakama ya juu yapewa Onyo

Jumatatu Mondlane aliionya mahakama ya juu, isithubutu kuyaidhinisha matokeo ya  urais yanayotiliwa shaka yaliyompa ushindi Chapo,na ikiwa itachukuwa uamuzi huo basi vurugu na ukosefu wa amani utashuhudiwa nchi nzima.

Kimsingi baraza la katiba ambacho ndio chombo cha juu cha maamuzi nchini Msumbiji, linatarajiwa kuyathibitisha matokeo yaliyokwisha tangazwa na tume baada ya uchaguzi.

Baraza hilo linatakiwa kisheria kuyathibitisha matokeo hayo alau wiki mbili kabla ya kuapishwa madarakani mgombea urais wa Frelimo Daniel Chapo , mnamo mwezi Januari, kuchukuwa nafasi ya rais anayeondoka Filipe Nyusi.Soma pia: Marekani, Uingereza na wengine walaani kuongezeka kwa machafuko Msumbiji

Tume ya uchaguzi ilimtangaza Chapo mshindi kwa kupata kiasi asilimia 71 ya kura wakati Venancio Mondlane mwenye umri wa miaka 50 anayekiongoza chama kidogo cha Podemos alichukuwa nafasi ya pili kwa kuchaguliwa na asilimia 20 ya wapiga kura.

Maandamano ya wafuasi wa upinzaniPicha: Jaime Alvaro/DW

Kwa mujibu wa Mondlane lakini, matokeo hayo ya tume sio ya kweli na anayapinga akisema hesabu zao za kura zinaonesha alipata asilimia 53 ya kura zilizopigwa huku Chapo akiambulia asilimia 36.   

Kutokana na hilo kiongozi huyo wa upinzani alionya jana kupitia tangazo lake alilolitoa kwa njia ya video akisema ikiwa ukweli utazingatiwa amani itakuwepo Msumbiji na ikiwa mamlaka zitaamuwa kukumbatia matokeo ya uwongo ya uchaguzi, basi nchi itatumbukia kwenye vurugu,na hali haitokuwa ya kawaida.

Amewataka wafuasi wake kuilemaza kabisa nchi hiyo kuanzia Jumatatu wiki ijayo,ambayo kwahakika ndiyo siku ya mwisho ya kuidhinisha matokea ya uchaguzi.

Waangalizi wa kimataifa walisema kwenye ripoti yao kwamba uchaguzi wa Oktoba ulikumbwa na dosari nyingi.

Maandamano ya upinzani tangu Oktoba

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imekuwa ikishuhudia machafuko yaliyosababisha kuuwawa kwa watu 130 kwa mujibu wa shirika la kiaraia la ndani la Plataforma Decide,ambalo pia takwimu zake ndizo zinazotajwa na shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International.Soma pia: Shirika la HRW: Askari wa Msumbiji wamewaua watoto 10

Maandamano mjini Maputo Novemba. 27.2024Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Lakini pia Mondlane ambaye ni mtangazaji wa zamani wa redio, amewataka wafuasi wake waanze wiki moja ya maombolezo kabla ya kuingia kwenye awamu mpya ya maandamano ya Jumatatu ijayo,ambayo ameapa, kwamba yatalemaza shughuli zote nchini humo.

Mashirika ya haki za binadamu yamezishutumu mamlaka za Msumbiji kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya waandamanaji katika nchi hiyo ambayo imekuwa ikitawaliwa na chama kimoja cha Frelimo tangu ilipopata Uhuru kutoka kwa Wareno mwaka 1975.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW