1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MONUSCO yaripoti kuongezeka kwa mauaji ya kiholela Congo

Caro Robi
25 Januari 2018

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO umeripoti kuongezeka kwa mauaji ya kiholela nchini humo hasa mwaka jana katika majimbo ya Kusini mwa nchi hiyo ya Kasai.

Proteste im Kongo
Picha: Reuters/K. Katombe

Katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu viwango vya ukiukaji wa haki za binadamu Congo, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa-MONUSCO umesema mwaka jana, vikosi vinavyohusishwa na serikali vilifanya mauaji ya kiholela ya watu 1,176 wakiwemo wanawake 89 na watoto 213.

Ikilaani mauaji hayo yaliyoongezeka nchini humo, MONUSCO imesema mauaji hayo ya kiholela yameongezeka mara tatu zaidi ya miaka miwili iliyopita. Majeshi ya Congo yanasemekana kusababisha karibu theluthi mbili ya vifo hivyo.

Mwaka jana, Visa 6,497 vya ukiukaji wa haki za binadamu na maovu mengine viliripotiwa kufanywa kote nchini humo sio tu na vikosi vya usalama vya serikali bali pia na makundi ya wapiganaji. Hiyo inamaanisha kuwa ongezeko la asilimia 25 ya visa kama hivyo vilivyoripotiwa mwaka 2016.

Congo yazongwa na mizozo

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, taifa lenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini na misitu, linazongwa na mizozo chungu nzima kuanzia ya kisiasa, kikabila pamoja na mzozo wa muda mrefu wa kukabiliana na makundi mengi ya waasi yaliyotapakaa nchini humo hasa katika eneo la mashariki mwa nchi.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Congo-MONUSCOPicha: Monusco/A.Khan

Ripoti hiyo ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo imezidi kufafanua kuwa ongezeko hilo la mauaji ya kiholela imetokana na mzozo usioonekana kuisha katika majimbo matatu yanayounda eneo la Kasai ambako watu 752 waliuawa.

Mzozo katika eneo hilo la Kasai ulizuka baada ya chifu Kamwina Nsapu aliyekuwa akimpinga Rais Joseph Kabila kuuawa mwezi Agosti mwaka 2016. Zaidi ya watu 3,000 wameuawa Kasai na wengine takriban milioni 1.4 wameyakimbia makazi yao tangu mzozo huo ulipoanza.

Kundi la wapiganaji wa Kamwina Nsapu linalaumiwa kwa kusababisha mauaji ya raia 79 wakiwemo wanawake saba na watoto tisa. Kundi jingine la waasi liitwalo Bana Mura ambalo wakati mwingine linashirikiana na wanajeshi wa Serikali liliwaua raia 67 wakiwemo wanawake tisa na watoto 21.

Wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa waliuawa mwezi Machi mwaka jana walipokuwa wakichunguza ghasia zinazojiri Kasai ambako Umoja wa Mataifa uligundua zaidi ya makaburi 80 yaliyozikwa watu wengi.

Kutoondoka madarakani kwa Kabila kwazidisha mzozo

Ripoti hiyo inakuja wakati ambapo Serikali ya Rais Joseph Kabila ikikandamiza maandamano kote nchini humo ya kumshinikiza kiongozi huyo aachie madaraka baada ya kuendelea kushikilia uongozi hata baada ya mihula yake ya kuhudumu kukamilika.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Jumapili iliyopita, watu sita waliuawa katika mji mkuu wa Kinshasa wakati wa maandamano yaliyoitishwa na Kanisa Katoliki kumshinikiza Rais Kabila kuondoka madarakani. Watu wengine zaidi ya hamsini walijeruhiwa na mamia kukamatwa na polisi. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa wito wa kuwepo amani Congo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka uchunguzi wa kina na wa kuaminika kufanywa kuchunguza mauaji hayo. MONUSCO imeushutumu utawala wa Congo kwa kukiuka na kuhujumu haki na uhuru wa raia wake kupitia mauaji, vitisho na maovu mengine ikiwemo kuwatishia wapinzani, wanahabari na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu katika juhudi za kuwanyamizisha.

Licha ya kuishitumu serikali ya Congo kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika ripoti yake, MONUSCO pia imeisifu serikali hiyo kupitia idara yake ya mahakama ikisema takriban wanajeshi 150 na polisi 51 walihukumiwa mwaka jana kwa makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Mwandishi: Caro Robi/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW