1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Kongo: MONUSCO yasitisha oparesheni zake jimbo la Kivu

Mitima Delachance2 Mei 2024

Tume ya amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO imesitisha operesheni zake za kulinda raia katika jimbo la Kivu kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia ombi la serikali.

DR Kongo | MONUSCO
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo MONUSCOPicha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Mamlaka ya ujumbe huo, ikiwa ni pamoja na jukumu lake la kulinda raia, inaishia katika jimbo hilo

Taarifa ya hivi karibuni ya Monusco inakumbusha kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kuondoa kikosi cha MONUSCO katika jimbo la Kivu Kusini Jumanne Aprili thelathini, kwa ombi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba MONUSCO ilianza kusitisha shughuli zake huko Kivu Kusini Januari mwaka huu.

Hata hivyo, Monusco imebaini kwamba idadi ndogo ya wafanyikazi wake waliovaa sare watabaki ili kuhakikisha usalama wa wafanyikazi wengine wa Umoja wa Mataifa, vifaa, misafara na kadhalika, hadi mwisho wa shughuli za kuondoka ifikapo Juni thelathini.

Soma pia:Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita, amesema jukumu la usalama na ulinzi wa kimwili wa raia katika jimbo hili sasa ni la vikosi vya ulinzi na usalama vya DRC.

"Baraza la Usalama liliitaka MONUSCO kuondoa askari wake Kivu Kusini ifikapo Aprili 30 na kuhamishia kazi hii ya kulinda raia kwa serikali." Alisema

Aidha alituma salamu zake za shukurani kwa raia na serikali ya Kongo kwa ushirikiano katika kipindi chote walipokuwa wakitekeleza majukumu yao.

"Ninasisitiza kwamba programu na mashirika ya Umoja wa Mataifa zitakuwa tayari kusaidia mamlaka za kitaifa na majimboni”

MONUSCO kukabidhi kambi kadhaa

Helkopta ya Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo MONUSCOPicha: Paul Lorgerie/DW

Miongoni mwa kambi za Monusco zilizokabidhiwa kwa mamlaka ya Kongo mna ile ya Kamanyola iliyomilikiwa na wapakistani katika bonde la mto Ruzizi iliyokabidhiwa kwa Polisi wa Kongo, kambi za wapakistani za Bunyakiri na Kabumu zilizokabidhiwa kwa jeshi la Kongo FARDC na kambi ya AMSAR iliyowahi kumilikiwa na askari wa amani wa Umoja wa mataifa kutoka Nchi ya China waliojihusisha hasa zaidi na kazi za ukarabati wa barabara na masuala ya afya ili kufanikisha shughuli za Monusco.

Mwanzo wa wiki hii, Monusco ilikabidhi vifaa kadhaa vya ukarabati wa barabara na kiafya kwa serikali ya jimbo la Kivu kusini vyenye thamani ya angalau dola milioni saba za Marekani. Kunasalia kambi za Mikenge, Minembwe, Rutemba, Uvira, Baraka na Sange ambazo nazo hivi karibuni zitakabidhiwa kwa jeshi la Congo.

Soma pia:Rais Felix Tshisekedi asema simu za kiganjani zina damu ya Wakongo

Waziri husika na miundombinu katika Jimbo la Kivu Kusini Gaston Cissa wa Numbe akiwa anahusika pia na mahusiano kati ya jimbo la Kivu kusini na MONUSCO amekumbusha kwamba kuondoka huko kwa ujumbe huo, kunafanyika wakati huu ambapo eneo la mashariki mwa nchi bado linaathiriwa na makabiliano ya M23 vinavyoungwa mkono na Nchi jirani ya Rwanda hata kama Rwanda imekuwa ikikanusha.

Aliwasihi maafisa wa MONUSCO kila mara kuweka shinikizo kwa jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhu la amani ya kudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

" Tunatumai kwamba mtaendelea kutetea Kongo ulimwenguni na kwamba siku moja tutaweza kuwatambua na hivyo kuwaadhibu wengine wote wanaoonekana na kushiriki bila kuchoka pamoja na Rwanda na M23 katika vurugu za amani na usalama na kupora rasilimali za nchi yetu”

Monusco imesema wafanyakazi wake wote waliovalia sare watarejeshwa makwao ifikapo Juni 30 na ni idadi ndogo zaidi ya wafanyikazi wa kiraia ndio watasalia na jukumu la kufanyia kazi mabadiliko hayo.

Imekumbusha pia kwamba Umoja wa mataifa utabaki nchini Kongo kupitia Mipango, Mifuko na programu zake mbalimbali.

Monusco inatarajiwa kuondoka kabisa Congo kikamilifu ifikapo Desemba mwaka huu.

Wakaazi Kivu washinikiza kuondolewa MONUSCO DRC

02:15

This browser does not support the video element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW