1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBolivia

Morales amtaka Arce kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri

24 Septemba 2024

Rais wa zamani wa Bolivia, Evo Morales, amemtaka rais wa sasa, Luis Arce, kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ndani ya kipindi cha masaa 24, vyenginevyo akabiliwe na ghadhabu za maelfu ya waandamanaji.

Bolivia Evo Morales
Rais wa zamani wa Bolivia, Evo Morales.Picha: Juan Karita/AP Photo/picture alliance

Morales aliwaongoza waandamanaji hao kwenye maandamano ya kilomita 190 kutoka kijiji cha Caracollo kuelekea mji mkuu, La Paz.

Kundi la waandamaji hao, wengi wao wakiwa wakaazi wa asili wa Bolivia, liliwasili kwenye viunga vya mji mkuu huo jioni ya jana, baada ya kushiriki kile walichokiita "maandamano ya miguu kuinurusu Bolivia, yaliyokumbana na mashambulizi ya wafuasi wa Arce yakiwa njiani.

Soma zaidi: Wafuasi wa rais wa zamani na wa sasa wapambana Bolivia

Akiwahutubia wafuasi wake, Morales alisema Wabolivia wamechoshwa na usaliti na ufisadi, kulindwa wasafirishaji wa madawa ya kulevya na usimamizi mbaya wa uchumi.

Akitowa sharti lake la mwisho kwa mrithi wake, Morales alisema ikiwa Lucho anataka kuendelea kutawala, basi lazima awabadilishe wale aliowaita mawaziri wa madawa ya kulevya, mafisadi na wabaguzi.

Lucho ni jina la utani la Rais Arce, ambaye aliwahi kuwa waziri wa uchumi chini ya Morales.