Morgan Tsvangirai atishia kuugomea uchaguzi wa rais
21 Machi 2008HARARE
Kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani nchini Zimbabwe na mgombea wa urais Moragan Tsvangira ametishia kujiondoa katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu ikiwa serikali itashindwa kufuata sheria za uchaguzi kuhusu zoezi la kuhesabu kura.
Serikali ya rais Robert Mugabe inapanga kuendesha zoezi hilo la kuhesabu kura za uchaguzi wa rais mahala pamoja wakati upinzani unataka shughuli hiyo ifanyike katika vituo vya kupigia kura.Aidha Tsvangira anadai kwamba tayari orodha ya madaftari ya wapiga kura imejazwa majina ya maelfu ya watu ambao hawako.Hii imetokea siku moja baada ya shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch kusema kwamba linaamini uchaguzi wa Zimbabwe hautakuwa wa haki wala huru.Shirika hilo lenye makao yake nchini Marekani linaishutumu serikali ya Mugabe kwa kupanga kuiba kura na kuwatisha wapinzani.