1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoMorocco

Morocco na Ufaransa zatinga nusu fainali ya Kombe la Dunia

11 Desemba 2022

Ufaransa na Morocco zimefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia baada ya kupata ushindi katika mechi mbili tofauti za robo fainali zilizochezwa Jumamosi.

FIFA Fußball WM 2022 in Katar | Marokko - Portugal
Picha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Mashabiki wa timu ya Ureno walijawa na huzuni baada ya timu yao waliyoishabikia kuondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwenye pambano na timu ya Morocco kwenye uwanja wa Al Thumami, mjini Doha nchini Qatar.

Morocco imeweka historia ya kuzifunga timu kubwa kwani kwenye michuano hiyo pia ilifaulu kifungisha virago timu ya Uhispania.

Mchezaji Youssef En-Nesyri alifunga bao la ushindi kwa Morocco katika dakika ya 42. Haijawahi kutokea taifa la Afrika kuingia kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia, lakini sasa Morocco ni fahari ya bara la Afrika.

Mchezaji maarufu wa timu ya Ureno Cristiano Ronaldo, mwenye umri wa miaka 37, aliondoka uwanjani huku akitokwa machozi mara baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa.

Ronaldo hakuwemo kwenye nusu ya kwanza kwenye mechi hiyo ya Jumamosi. Mchezaji huyo nyota aliyejinyakulia tuzo ya mchezaji bora wa mwaka (Ballon d´Or ) mara tano aliwekwa benchi kama mchezaji wa akiba na kocha wa Ureno akaamua kumuingiza uwanjani katika nusu ya pili kwenye dakika ya 51.

Hata hivyo Ronaldo alipopata nafasi ya kulishambulia lango la Morocco hakufaulu kupenyeza mpira kimiani.

Salamu za pongezi zamimika kwenda kwa timu ya Morocco 

Wachezaji wa timu ya taifa ya Morocco wakishangilia ushindi dhidi ya Ureno Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Kufuatia ushindi huo wa Morocco, viongozi wa kisiasa, watu mashuhuri na nyota kadhaa wa michezo wametuma salamu za pongezi na kuimwagia sifa timu hiyo.

Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby na mfalme Hamad Al Khalifa wa Bahrain wameutaja ushindi wa Morocco dhidi ya Ureno kuwa wa "kihistoria" baada ya timu hiyo kuwa ya kwanza kutoka barani Afrika na kwenye ulimwengu wa kiarabu kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya kandanda.

Salamu nyingine za pongezi kwa timu hiyo inayofahamika pia kama "simba wa milima ya Atlas" zimetolewa na viongozi wa Dubai, Libya, Palestina, Iraq, Jordan, Misri na wachezaji mashuhuri wa zamani akiwemo Samuel Etoo wa Cameroon.

England yakusanya virago baada ya Ufaransa kusonga mbele 

Picha: Keita Iijima/AP/picture alliance

Kwingineko timu ya Uingereza ilifungwa mabao 2-1 kwenye pambano la kusisimua ilipokutana na timu ya Ufaransa. Timu hizo zilicheza kwenye uwanja wa Al Bayt uliojaa mashabiki. Magoli ya Ufaransa yalifungwa na Aurelien Tchouameni na Olivier Giroud.

Olivier Giroud amesema timu ya Ufaransa ililazimika kutumia akili ili kuung'nga'nia ushindi wa 2-1 dhidi ya Uingereza katika michuano ya robo fainali ya Kombe la Dunia.

Kwa upande wa Uingereza mchezaji Harry Kane alikosa nafasi ya dakika za mwisho ya kusawazisha kwa mkwaju wa penati.

Ufaransa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia sasa watakutana na Morocco kwenye nusu fainali.

Kwa matokeo hayo Ufaransa itapambana na Morocco wiki inayokuja kwa mchezo wa nusu fainali. Mchezo mwingine wa nusu fainali utazikutanisha Argentina na Croatia ambazo tayari zilisonga mbele siku ya Ijumaa.