Morocco yachaguliwa rais wa baraza la haki za binadamu 2024
10 Januari 2024Omar Zniber ameshinda kura 30 katika kinyang'anyiro na balozi wa Afrika Kusini, Mxolisi Nkos, ambaye amepata kura 17.
Ilikuwa zamu ya bara la Afrika kuchukua urais wa baraza hilo lakini nchi za Afrika hazikuweza kukubaliana juu ya mgombea mmoja kutoka kwa jumla ya wanachama 13 wa baraza hilo, ndio maana kukafanyika kura ya siri.
Soma pia: EU, AU wakubaliana kuimarisha ushirikiano
Baada ya kushinda, Zniber amesema kazi ya baraza hilo ni muhimu na ni ya msingi: kulinda na kuheshimu haki za binadamu kama zinavyotambulika kimataifa.
Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilianzishwa mnamo 2006 na lina kazi ya kulinda, kuendeleza haki za binadamu kote ulimwenguni na kushughulikia vitendo vya ukiukaji.
Urais wake huzunguka kila mwaka kati ya makundi matano ya baraza hilo.