Moscow. Ndege za misaada zaenda Marekani.
6 Septemba 2005Ndege mbili za kwanza kubwa za kubebea mizigo kutoka Russia , zikiwa zimebeba bidhaa mbali mbali za misaada kwa ajili ya wahanga wa kimbunga Katrina , zinasubiri kupewa kibali na Marekani ili kuweza kuondoka nchini himo, waziri anayehusika na masuala ya tahadhari amesema leo.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Russia Veronika Smolskaya amesema kuwa wizara yake inajadiliana na maafisa wa Marekani juu ya viwanja ambapo ndege hizo zitatua.
Baada ya Russia kukataliwa na Marekani kupeleka vikosi vya uokozi pamoja na misaada mingine , wizara ya hali ya tahadhari imesema jana kuwa viongozi wa Marekani wamekubali Russia ipeleke misaada ya kibinadamu katika eneo hilo lililokumbwa na maafa ya kimbunga Katrina.
Wakati huo huo Ujerumani inatarajiwa kutoa zaidi ya mapipa milioni 3.3 ya mafuta ghafi kusaidia kuinua kiwango cha upatikanaji wa mafuta baada ya kimbunga Katrina kuharibu baadhi ya vinu na maeneo ya uhifadhi wa mafuta.
Waziri wa uchumi Wolfgang Clement ametangaza hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya uratibu wa hatua ya mataifa 26 wanachama wa shirika la kimataifa la nishati kukubali kutoa kiwango hicho cha mafuta katika soko la dunia.
Clement amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya Ujerumani kujiunga na juhudi za kimataifa za mshikamano na raia wa Marekani ambao wameathirika na kimbunga Katrina.
Clement pia amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza mbinyo uliopo katika bei ya mafuta, ambayo imepanda tena wiki iliyopita baada ya kimbunga Katrina kuharibu vinu vya kusafishia mafuta vya Marekani katika ghuba ya Mexico.