Moto Los Angeles: Watu 10 wauawa, maelfu ya nyumba zateketea
10 Januari 2025Kando na vifo hivyo, hadi sasa, takriban watu 360,000 wamehamishwa kutoka maeneo hayo ya hatari hadi maeneo salama.
Moto mkubwa unaoendelea umeripotiwa kwamba umeshateketeza takriban hekari 8,000 eneo la Palisades viungani mwa mji wa Los Angeles. Kulingana na idara ya kuzima moto ya Los Angeles, asilimia 6 pekee ya moto huo ndiyo imezimwa hadi ilipotimia saa tatu usiku majira ya Marekani. Huo ni mkasa mmoja tu wa zaidi ya mikasa mitano inayoendelea kusababisha maafa nchini Marekani.
Nao moto kule eneo la Eaton, viungani mwa Los Angeles pia umesambaa na kuteketeza zaidi ya hekari 5,500 na haujadhibitiwa hata kidogo.
Kulingana na afisa mkuu wa wazima moto wa Los Angeles Kristin Crowley, tangu Jumanne wiki hii, zaidi ya nyumba 5, 300 zimeteketezwa moto katika mitaa ya Pasifiki Palisades, viungani mwa mji wa Los Angeles.
Rais Biden atangaza msaada kukabili moto Los Angeles
Mnamo Alhamisi Alhamisi, rais wa Marekani Joe Biden alisema moto huo ndio mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya jimbo hilo lililoko magharibi mwa Marekani. Biden alitangaza msaada zaidi kusaidia kukabili janga hilo.
Mnamo mwaka 2024, moto wa nyikani ulichoma eneo lenye ukubwa wa ekari 370,000 huko California.
Unaweza kusoma pia: Moto wa nyika unaoshika kasi waharibu majengo huko Los Angeles
"Ndiyo mikasa mibaya zaidi ya moto kuwahi kuikumba Los Angeles. Na punde ilipozuka niliidhinisha msaada wa kudhibiti moto wa jinsi ya kusaidia. Misaada hii itashughulikia gharama zote za kupambana na Mikasa hii ya moto jimbo la California,” amesema Biden.
Naye mkuu wa kupambana na moto wa kaunti ya Los Angeles Anthony Marrone, amesema kati ya majengo 4,000 hadi 5,000 yakiwemo ya kibiashara na majengo binafsi ya kifahari yameharibiwa na moto huo katika mtaa wa Eaton karibu na Pasadena.
Ukosefu wa mvua kwa miezi minane
Wazima moto wamefanikiwa kuzima moto katika maeneo mawili ya West Hills na Hidden Hills yaliyoko kati ya Los Angeles na Ventura.
Kulingana na Gavana wa California Gavin Newsom, maafisa 900 zaidi wa kupambana na moto watatumwa kupiga jeki juhudi hizo.
Hii si mara ya kwanza kwa jimbo la California Marekani kukumbwa na majanga ya moto wa nyikani.
Unaweza kusoma pia: Maelfu watumwa kuukabili moto wa nyika California
Mvua haijanyesha eneo hilo la kusini mwa California kwa miezi isiyopungua minane mfululizo, hivyo kusababisha miti na vichaka kukauka. Kitu kingine ambacho kinasababisha mioto hiyo kuenea kwa kasi ni upepo wa Santa Ana unaovuma kwa kasi.
Makadirio ya hasara
Kulingana na makadirio ya awali yaliyofanywa na shirika binafsi la utabiri wa hali ya hewa Accuweather, na ambalo pia hupima athari za hali mbaya zaidi za hewa, hasara iliyosababishwa na Mikasa hiyo ya moto inaweza kuwa kati ya dola bilioni 135 na dola bilioni 150.
Unaweza pia kusoma: Watu 76 wafa, zaidi ya 1,000 hawajulikani walipo moto wa California
Miongoni mwa hasara hizo ni pamoja na maelfu ya nyumba na majengo yaliyoharibiwa, miundo mbinu na ujenzi upya na utoaji huduma utakaofuata. Lakini maadamu mioto yote haijazimwa, huenda makadirio hayo yakaongezeka.
Kulingana na vyombo vya habari nchini humo, kufikia sasa, takriban majengo 10,000 yameteketezwa moto.
(DPAE)