Moto wauteketeza mji wa kihostoria Lahaina
11 Agosti 2023Moto wa nyika ulioteketeza kisiwa cha Maui kilichopo Hawaii umeteketeza pia mji wa kihistoria wa Lahaina. Huku juhudi za utafutaji na uokoaji zikiendelea, Idadi ya waliofariki inakadiriwa kuongezeka zaidi.
Idadi ya watu waliofariki kutokana na janga la moto katika kisiwa cha Maui cha Hawaii nchini Marekani imeongezeka hadi 55. Kwa mujibu wa mamlaka visiwani humo, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka huku juhudi za utafutaji na uokoaji zikiendelea kufanyika na vikosi vya zima moto bado walikuwa wakipambana na moto huo kote visiwani.
Hii ni mojawapo ya maafa mabaya zaidi katika historia ya jimbo la Marekani ambapo moto huo umepelekea mateso na uharibifu mkubwa, huku maelfu ya watu wakihama makazi yao na majengo kuharibiwa.
Mji wa kihistoria wa Lahaina uliharibiwa
Moto huo ulianza Jumanne na ulichochewa na upepo mkali, huku chanzo chake mpaka sasa bado hakijabainishwa, ulienea kwa haraka na umeteketeza mji wa kihistoria wa pwani Lahaina ambao pia umekua ni kivutio kikuu cha watalii, mji wa Lahaina ambao hapo awali ulikuwa mji mkuu wa Ufalme wa Hawaii, ulikua na wakaazi wapatao 12,000
Kufuatia tukio hilo Gavana wa Hawaii Josh Green amesema, Itachukua miaka mingi kujenga upya Lahaina, sababu asilimia 80 ya mji imeteketea. Itakuwa Lahaina mpya ambayo Maui iliijenga kwa taswira yake, liliyovutia watalii milioni 2 kila mwaka kuja visiwani humo.
Soma zaidi: Watu 36 wafariki kutokana na moto mkali kwenye Visiwa vya Hawaii
Wakazi wa Lahaina waliambia shirika la habari la AFP kwamba baadhi yao waliweza kuchukua nguo za kubadilisha tu na kukimbia na watoto pindi vichaka vilivyowazunguka vikiwaka moto, na hawana uhakika kama kuna kitu chochote kilichosalia katika nyumba zao.
Nae Brandon Wilson, raia wa Kanada amesema kwa jinis tukio linavyoonekana, ni kama kuna mtu alikuja na kushambulia mji mzima kwa mabomu, kwa jinsi ambavyo kumeharibia.
Nae Profesa katika Idara ya Sayansi ya Anga katika Chuo Kikuu cha Hawaii, Steven Businger, ameiambia DW, upepo mkali uliovumishwa na dhoruba Kaskazini mwa visiwa vya Hawaii uliuzidisha moto na kuwaunguza watu wakati wa usiku wakiwa wamelala pasipo kutarajia.
Je, juhudi za uokoaji na msaada zikoje?
Changamoto kadhaa zimelikumba eneo hilo ikiwemo kukatika kwa umeme na kukatika kwa huduma za simu katika sehemu za kisiwa hicho. Maelfu ya watalii na wenyeji tayari wamehamishwa, na juhudi za uokoaji na kutoa misaada zinaendelea. Ambapo Mkuu wa huduma ya zimamoto Brad Ventura ameshauri watu kukaa mbali na eneo linaloteketea kwani bado ameeleza ni hatari.
Wakati hayo yakiendelea Rais wa Marekani Joe Biden amesema moto huo ni "janga kubwa," na ameahidi kutoa fedha za shirikisho kuisaidia Maui. Rais biden pia ametuma timu za utafutaji na uokoaji kutoka California na jimbo la Washington kusaidia katika mchakato huo.
Soma zaidi: Mioto iliyokuwa ikiwaka kwenye sehemu mbalimbali za Ugiriki imedhibitiwa leo Jumatano
Nae mkuu wa polisi wa Maui John Pelletier ametoa wito wa watu kuwa na subira na uvumilivu na kuwataka wasali katika kipindi hiki ambacho mji wa Lahaina umeteketea, na ameeleza mabaki ambayo bado hayajapatikana ni lazima wayatoe.
Moto huchochewa na mabadiliko ya hali ya hewa
Mwenyekiti wa zamani wa Jopo la Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) Robert Watson, amesema kutokana na mabadiliko ya mifumo ya mvua, kumekua na mafuriko katika baadhi ya maeneo. Pia ukame katika maeneo mengine kutokana na misitu mbalimbali kuwa mikavu, hivyo mabadiliko ya hali ya hewa yanachochea hatari ya moto wa nyikani kote duniani.
Watson ametolea mifano ya yale yaliyowahi kutokea nchi za Kanada, Ugiriki na sasa Hawaii. Ameongeza kusema hizo ni aina za athari ambazo tunaweza kuziona katika misitu kote ulimwenguni.
Moto huo unafuatia matukio mengine mabaya ya hali ya hewa kuwahi kutokea Amerika Kaskazini, huku eneo hilo likishuhudia wimbi la joto kali na moto uliovunja rekodi.