1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa hekalu wauwa 100 India

10 Aprili 2016

Moto na miripuko iliyotokea Jumapili (10.04.2016) wakati wa maonyesho ya fataki kuadhimisha mwaka mpya kwa Wahindu imeuwa watu 100 na kujeruhi wengine 380 kwenye hekalu katika jimbo la kusini la Kerala nchini India.

Watu wakiwa wamekusanyika nje ya hekalu la Kolam lililoshika moto katika jimbo la Kerala India. (10.04.2016)
Watu wakiwa wamekusanyika nje ya hekalu la Kolam lililoshika moto katika jimbo la Kerala India. (10.04.2016)Picha: Reuters/Sivaram V

Moto na miripuko iliyotokea Jumapili (10.04.2016) wakati wa maonyesho ya fataki kuadhimisha kuanza kwa mwaka mpya kwa Wahindu imesababisha watu 100 kupoteza maisha yao na kujeruhi wengine 380 kwenye hekalu lilioko katika jimbo la kusini la Kerala nchini India.

Maelfu ya wafuasi wa dini ya Kihindu walikuwa wamefurika katika hekalu la Puttingal Devi lilioko kama kilomita 70 kutoka mji mkuu wa jimbo Thiruvananthapuram katika kitongoji cha mwambao cha Kollam kuangalia maonyesho hayo yaliyoanza usiku wa manane na kudumu kwa masaa manne.

Moto huo ulianza wakati fataki ilipoangukia kwenye kibanda ambacho kilikuwa kimehifadhi fataki na kusababisha mfulululizo wa miripuko mikubwa ambayo iliangusha paa la ofisi ya utawala ya hekalu hilo pamoja na kungusha jengo jengine.

Kwa mujibu wa mkaazi mmoja Anita Prakash sehemu za miili zilikuwa zimezagaa kwenye sakafu na kwamba huko nyuma kumewahi kuwepo kwa maonyesho ya fataki lakini hayakuwa makubwa kufikia kiwango hiki.

Kuna mahekalu mengi huko Kerala yanayosimamiwa na udhamini wa matajiri wenye ushawishi mkubwa ambao mara nyingi wamekuwa wakikiuka taratibu za serikali za mitaa.Kila mwaka mahekalu huwa yanafanya maonyesho ya fataki na mara nyingi hushindana baina yao kufanya maonyesho ya kutia fora ambapo majaji huamuwa mshindi.

Hakimu wa wilaya ya Kollam A. Shainamol amesema watu wanaoishi katika eneo karibu na hekalu huko nyuma wamekuwa wakilalamika juu ya hatari za fataki hizo.

Waziri Mkuu azuru eneo la maafa

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amekwenda Kollam na timu ya madaktari kusaidia maafisa wa serikali ya jimbo kukabiliana na idadi kubwa ya majeruhi akichukuwa hatua haraka kwa lengo la kuzima shutuma juu ya uhaba wa usalama wa umma.

Sehemu ya hekalu la Kolam ilioteketezwa.Picha: Reuters/Sivaram V

Amekaririwa akisema katika mtandao wake wa Twitter "Moto uliozuka katika hekalu huko Kollam ni wa kusononesha na kushtuwa kushindwa kuelezeka kwa maneno." Amesema anaungana na familia za wahanga na majeruhi kwa maombi.

Modi alikabiliwa na shutuma za umma huko nyuma kwa kushindwa kuchukuwa hatua za haraka wakati wa maafa kama vile mafuriko huko Chennai mwishoni mwa mwaka jana. Sehemu kubwa ya jiji hilo kubwa lilikuwa ndani ya maji kabla ya kuwasili kwa msaada wa serikali.

Maafa ya ajali

Mapema mwaka huu njia ya juu ya ardhi iliokuwa ikiendelea kujengwa kwa miaka mingi katika mji wa mashariki wa Kolkata ilianguka na kuuwa watu 27 na kuzusha madai ya kutumika kwa vifaa dhaifu na kwamba vilikuwa tayari vimechakaa kutokana na kucheleweshwa kwa ujenzi huo kwa miaka mingi.

Watu wakiwa wamekusanyika nje ya hekalu la Kolam lililoshika moto katika jimbo la Kerala India. (10.04.2016)Picha: Reuters/Sivaram V

Picha za tekevisheni kutoka eneo la hekalu lililoteketezwa imeonyesha watu wengine wamebeba watoto wenye majeraha ya moto wakipelekwa hospitali.Wengine walikuwa wamebeba miili ya wahanga waliounguwa.

Waziri wa mambo ya ndani wa Kerala Ramesh Chennithala ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba watu 60 kati ya 100 waliouwawa wametambulika wakati watu waliolazwa hospitali huko Kollam na mji mkuu wa jimbo imeongezeka na kufikia 383.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters

Mhariri : Sudi Mnette

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW