1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa msituni watishia miundombinu Ugiriki na Uturuki

Daniel Gakuba
5 Agosti 2021

Wazimamoto nchini Uturuki, Ugiriki na mataifa mengine ya ukanda wa bahari ya Mediterania kusini mwa Ulaya wanapambana na moto wa msituni, unaoenea kwa kasi na kutishia miundombinu muhimu na maeneo ya kihistoria.

Türkei Waldbrände
Moto karibu na kituo cha kufua umeme nchini UturukiPicha: Turan Salcı/Sputnik/dpa/picture alliance

Asubuhi ya leo, hofu ilikuwa imeenea nchini Uturuki kuwa moto huo unaoteketeza misitu kwa zaidi ya wiki moja sasa ulikuwa umefika katika eneo la mtambo muhimu wa kufua umeme wa Kemerkoy ulio kusini magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa twitter, Fahrettin Altun, mkurugenzi wa mawasiliano wa ofisi ya rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema tathmini ya mwanzo inaonyesha kuwa mtambo huo haukuharibika sana.

Wafanyakazi kwenye mtambo huo pamoja na wakaazi wa maeneo ya karibu waliokolewa kwa kutumia meli ya kijeshi, wakati ndimi za moto zilipokuwa zikienea haraka kutokana na upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi.

Wanaharakati wa kulinda mazingira walikuwa wametabiri kuwa kuungua kwa mtambo huo wa umeme unaotumia makaa ya mawe, kungekuwa na athari mbaya kabisa.

Baadhi ya wakaazi wa maeneo yaliyoathirika wamepoteza kila kituPicha: Ali Balli/AA/picture alliance

Kilio cha wahanga hakisikiki

Takribani maeneo 160 yameunguzwa kabisa na moto na kubakia majivu nchini Uturuki.

''Historia ya mababu zetu imeteketea, kumbukumbu ya utoto wangu imeangamizwa, pamoja na mustakabali wa watoto wetu, kila kitu kimeungua,'' amesema mmoja wa wazimamoto wa kujitolea, Ummuhan Saglam Karayel, na kuongeza ''Tumepaaza sauti lakini hatusikiki. Tumelia hakuna anayetusikiliza.''

Nchini Ugiriki nako shughuli ya kupambana na moto huo wa msituni inaendelea kwa siku ya tatu mfululizo, huku maafisa wa serikali wakiwataka wakaazi wa visiwa vya karibu na mji mkuu, Athens kuondoka.

Leo hii kazi kubwa ilikuwa ni kukinusuru kituo cha kale cha michezo ya Olimpiki magharibi mwa mkoa wa Peloponnese.

Mojawapo ya vijiji vilivyoteketezwa na motoPicha: YASIN AKGUL/AFP

Jinamizi ambalo mwisho wake hauonekani

Shughuli hii inawahusisha wazimamoto 170, wanaosaidiwa na magari maalumu yapatayo 52 pamoja na ndege sita. Waziri wa usalama wa raia Mihalis Chrisohoidis amekiambia kituo kimoja cha televisheni, kuwa watu hao wamepambana usiku kucha bila kupumzika.

Huku nako moto umeripuka katika maeneo zaidi ya 150, ukichochewa na joto kali la zaidi ya nyuzi 45 za celsius, na upepo unaovuma kwa kasi. Magazeti ya Ugiriki yanalielezea janga hili la moto wa msituni kama jinamizi ambalo mwisho wake haujulikani.

Nchi kadhaa nyingine za Ulaya zinazopakana na bahari ya Mediterania, zikiwemo Italia, Albania na Macedonia Kaskazini pia zimekumbwa na janga hili la moto wa msituni, na kitengo cha Umoja wa Ulaya cha kupambana na majanga kimesema kinapeleka msaada wa ndege na wataalamu wa kuzima moto.

 

ape,rtre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW