1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaKenya

Wanafunzi 16 wafariki moto wa shule ya bweni Kenya

Wakio Mbogho ape,rtre
28 Mei 2026

Waziri wa Elimu wa Kenya Migos Ogamba amethibitisha kuwa wanafunzi 16 wamefariki kutokana na moto uliozuka majira ya alfajiri siku ya Jumatano katika bweni ambalo lilikuwa na takriban wanafunzi 220 waliokuwa wamelala.

Kenya, Nairobi 2024 | Zimamoto katika eneo la mlipuko wa gesi mtaa wa Embakasi
Baada ya moto mbaya wa mwaka 2024, serikali iliahidi kufanya ukaguzi wa usalama katika shule zote na kuwachukulia hatua waliokiuka sheria, lakini bado haijafahamika wazi kama hatua hizo zilitekelezwaPicha: Joy Nabukewa/Xinhua/IMAGO

Wanafunzi wasiopungua 16 wamefariki dunia baada ya moto kuzuka usiku katika bweni la shule ya wasichana nchini Kenya, katika tukio jingine la moto wa shule lililoishtua nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Waziri wa Elimu wa Kenya Julius Ogamba amesema Alhamisi kuwa wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa katika shule ya Utumishi Girls School iliyopo eneo la Gilgil katikati mwa Kenya.

Moto huo ulizuka muda mfupi kabla ya saa saba usiku kwa saa za huko katika shule hiyo iliyoko Kaunti ya Nakuru, takribani kilomita 120 kutoka mji mkuu Nairobi.

Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika. Ogamba amesema mamlaka zitachunguza iwapo taratibu za usalama dhidi ya moto zilizingatiwa shuleni hapo.

Polisi walisema wanaongoza juhudi za uokoaji na huduma za dharura katika shule hiyo inayomilikiwa na serikali na kusimamiwa na Huduma ya Polisi Kenya.

Hapo awali, watoto wamewahi kutuhumiwa kwa kuwasha moto mashuleni kwa makusudi. Ripoti moja ilibaini kuwa kulikuwa na visa 63 vya uchomaji moto mashuleni mwaka 2018 pekeePicha: Gerald Anderson/Anadolu Agency/IMAGO

Serikali yaanza uchunguzi wa chanzo cha moto

Wanafunzi wengi katika shule hiyo ni watoto wa maafisa wa polisi. Hadi sasa miili ya waliofariki bado haijatambuliwa rasmi.

Mzazi mmoja aliyekuwa eneo la tukio, Wambui Nderitu, alisema mlezi wa bweni alifungua moja ya milango miwili ya bweni bila kuwaelekeza wanafunzi kutoka haraka.

"Mlango wa pili uliendelea kufungwa. Ingawa binamu yangu alinusurika akiwa amejeruhiwa mguuni, tumeambiwa watoto wengi wamejeruhiwa na wengine wamefariki,” alisema Nderitu.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema wanafunzi kadhaa waliokolewa na kupelekwa katika hospitali mbalimbali kwa matibabu.

Shirika hilo pia lilisema limetuma timu za msaada wa kisaikolojia na za kusaidia familia kutambua waliopotea.

Historia ya moto wa shule yaendelea kuitikisa Kenya

Rais wa Kenya William Ruto ametaja tukio hilo kuwa "janga lisilofikirika” na kutuma salamu za pole kwa familia zilizopoteza watoto wao.

Kenya imewahi kushuhudia matukio mengine mabaya ya moto mashuleni katika miaka iliyopita. Moto mbaya zaidi ulitokea mwaka 2001 katika Kaunti ya Machakos ambapo wanafunzi 67 walifariki katika bweni la shule.

Mwaka 2024, wanafunzi 21 walifariki baada ya moto kuteketeza bweni katika shule ya Hillside Endarasha Academy kaunti ya Nyeri, huku serikali ikiahidi kufanya ukaguzi wa usalama katika shule zote nchini.

Ripoti ya mwaka 2017 ya Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Uhalifu Kenya ilieleza kuwa msongo wa mitihani, mihula mirefu ya masomo na mawasiliano ya wanafunzi kupitia simu zilizofichwa vilichangia baadhi ya matukio ya uchomaji moto mashuleni.

Maafisa wa serikali wamewataka wananchi kusubiri matokeo ya uchunguzi huku wakionya dhidi ya uvumi kuhusu chanzo cha moto huo.

Usalama wa wanafunzi katika shule za bweni Kenya

02:37

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW