Moto wateketeza ghala la tume ya uchaguzi Congo
13 Desemba 2018Moto huo ulioripotiwa Desemba 13 saa nane usiku mjini Kinshasa, umeteketeza zaidi ya kompyuta elfu saba za kupigia kura, pamoja na vifaa vingine vya uchaguzi na magari kadhaa ya kusafirishia vifaa hivyo.
Moto huo unaoaminika na viongozi wa Kongo kuwa ni wa kihalifu, uliteketeza ghala hilo kwa zaidi ya kipindi cha masaa manne kabla maafisa wa kitengo cha zima moto kuuzima.
Mwenye kiti wa tume huru ya uchaguzi CENI, Corneille Nangaa ambaye amelitembelea eneo la tukio hilo amesema uharibifu ni mkubwa.
"Ukweli ni kwamba moto uliteketeza mojawapo ya maghala yetu ya CENI ambako kuliwekwa vifaa vya uchaguzi vya mji wa Kinshasa. Tumeanza tathmini ili kufahamu ukubwa wa uharibifu lakini bila shaka kisa hichi kitaathiri taratibu ya uchaguzi lakini haitositisha taratibu nzima" amesema Corneille Nangaa.
Tume huru ya uchaguzi imesema kwamba ni mapema mno kufahamu chanzo na sababu za moto huo na vilevile ukubwa wa madhara yaliyotokea.
Mshauri wa maswala ya kidiplomasia wa Rais Joseph Kabila, Kikaya bin Karubi amesema kwamba zaidi ya kompyuta 7,000 zilizotakiwa kutumiwa kwa ajili ya uchaguzi wa mji wa Kinshasa zimeunguwa. Huku akiwanyooshea kidole cha lawama wale aliowaita kuwa ni maadui wa demokrasia ambao walifanya kitendo hicho.
Matumizi ya mashine yazuwa utata
Matumizi ya kompyuta kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa Desemba 23, yamezusha tofauti kubwa hadi sasa. Baadhi ya wapinzani wametupilia mbali matumizi hayo na kusema yameandaliwa na serikali ya rais Kabila kwa ajili ya kuiba kura.
Waziri wa mambo ya ndani, Henri Mova Sakanyi amesema kwamba ni takriban asilimia 10 ya vifaa vya uchaguzi mjini Kinshasa vilivyoungua na kuhakikisha kwamba vifaa vingine vitabadilishwa haraka iwezekanavyo. Mova amesema kwamba uchunguzi unaendeshwa kufahamu sababu za tukio hilo, na kwamba huenda ikawa ni kisa cha uhalifu na waliojaribu hilo hawakufanikiwa.
zimesalia siku kumi kabla ya kumalizika kwa kampeni za uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini kampeni hizo zimekumbwa na visa kadhaa vya umwagikaji wa damu, uharibifu na vitisho baina ya wagombea. Wapinzani wao kwa wao wamelaumiana na vilevile kumlaumu mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, huku naye akiwalaumu wapinzani kwamba wamepanga vurugu kwa ajili ya kupinga matokeo ya uchaguzi.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo
Mhariri: Josephat Charo