1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
KandandaAfrika

CAF: Uwekezaji umezaa matunda kwa soka la Afrika

29 Juni 2026

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, Patrice Motsepe, amesema mafanikio ya timu tisa za Afrika kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu katika vijana, makocha na miundombinu.

Algeria Algiers 2022 | Mkutano na waandishi wa habari wa Rais wa CAF Patrice Motsepe
Motsepe anasema uwekezaji katika soka la vijana, mafunzo ya makocha, ligi za kitaalamu na miundombinu umechangia mafanikio ya sasa ya mataifa ya Afrika katika Kombe la DuniaPicha: Wu Tianyu/Xinhua/IMAGO

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema mafanikio ya timu za Afrika katika Kombe la Dunia 2026 yanaonyesha matunda ya uwekezaji wa muda mrefu katika maendeleo ya soka barani humo.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa hatua ya makundi, Motsepe alisema uwekezaji katika soka la vijana, mafunzo ya makocha, ligi za kitaalamu na miundombinu umechangia mafanikio ya sasa ya mataifa ya Afrika.

Timu tisa kati ya kumi zilizowakilisha Afrika zimefanikiwa kufuzu hatua ya 32 bora ya mashindano yanayoendelea Marekani, Canada na Mexico.

Algeria, Cape Verde, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ghana, Côte d'Ivoire, Morocco, Senegal na Afrika Kusini zimefuzu hatua ya mtoano, huku Tunisia ikiwa timu pekee iliyoshindwa kusonga mbele baada ya kupoteza mechi zake zote tatu.

Motsepe aliwapongeza marais wa vyama vya soka vya mataifa hayo pamoja na kamati zao za utendaji, huku pia akizishukuru serikali za Afrika kwa ushirikiano na msaada waliotoa katika kuendeleza mchezo huo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiyo timu pekee kutoka Kanda ya Maziwa Makuu inayoshiriki Kombe la DuniaPicha: Eloisa Sanchez/REUTERS

Utawala bora na uwekezaji

Rais huyo wa CAF alisema maboresho katika utawala, uwazi, usimamizi wa fedha na ukaguzi wa hesabu yamevutia wafadhili na washirika wapya, hatua iliyosaidia kukuza soka la Afrika.

Aliongeza kuwa CAF ina matumaini makubwa kwamba timu hizo tisa zitaendelea kufanya vizuri na kuziwakilisha nchi zao pamoja na bara la Afrika kwa heshima katika hatua ya mtoano.

Kwa mujibu wa takwimu za mashindano, Afrika imekuwa bara lililofanya vizuri zaidi katika hatua ya makundi kwa kufanikisha asilimia 90 ya timu zake kufuzu hatua ya pili.

Amerika Kusini imefuata kwa asilimia 83.3, huku Ulaya ikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 81.25 ya timu zake kufuzu.

Safari ndefu ya Afrika kusaka ubingwa wa Kombe la Dunia

03:46

This browser does not support the video element.

Cape Verde yaendeleza hadithi ya mafanikio

Motsepe amesema mafanikio hayo yanathibitisha kuwa soka la Afrika linaendelea kukua na lina uwezo wa kushindana na mataifa makubwa duniani.

Moja ya hadithi kubwa za mashindano ni Cape Verde, taifa la visiwa lenye wakazi zaidi kidogo ya nusu milioni, ambalo limefuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Cape Verde ilianza safari yake kwa kuishangaza Cameroon katika mechi za kufuzu, kabla ya kutoka sare dhidi ya Hispania, Uruguay na Saudi Arabia katika hatua ya makundi na kumaliza katika nafasi ya pili ya Kundi H.

Morocco yaendelea kuhamasisha bara

Motsepe amesema mafanikio ya Morocco ya kufika nusu fainali mwaka 2022 yalitoa imani mpya kwa mataifa mengine ya Afrika kwamba yanaweza kushindana kwa mafanikio katika Kombe la Dunia.

Alikumbusha kuwa Morocco iliwaondoa Ubelgiji, Hispania na Ureno kabla ya kutolewa na Ufaransa katika nusu fainali ya mashindano yaliyofanyika Qatar.

Afrika yaweka historia Soka la wanawake duniani

02:21

This browser does not support the video element.

Afrika ilinufaika na uamuzi wa FIFA kupanua Kombe la Dunia kutoka timu 32 hadi 48, na kupata nafasi tisa za moja kwa moja huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiongeza idadi hiyo hadi kumi baada ya kushinda mchujo wa mabara dhidi ya Jamaica.

Kwa mafanikio hayo, Motsepe amesema Afrika sasa ina kila sababu ya kuamini kuwa siku ya bara hilo kutwaa Kombe la Dunia inazidi kusogea.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW