Mourinho kutumikia kifungo cha nje kwa ukwepaji kodi
5 Februari 2019Kocha wa zamani wa klabu ya kandanda ya Real Madrid na Manchester United Jose Mourinho amepewa hukumu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kukubali kuwa ana hatia kwa udanganyifu wa kodi nchini Uhispania siku ya Jumanne.
Mourinho hatatumikia kifungo jela baada ya kukiri kufanya udanganyifu kwa maafisa wa Uhispania mwaka 2011 na mwaka 2012.
Hukumu ya miaka miwili ama chini ya hapo kwa watu waliofanya makosa kwa mara ya kwanza inaweza kusitishwa nchini Uhispania. Mourinho alifika mbele ya jaji katika mahakama mjini Madrid kuthibitisha makubaliano ya kukubali kosa aliyofikia na waendesha mashitaka. Kama sehemu ya mpango huo pia atawajibika kulipa faini ya euro milioni 2.
Kocha huyo nyota raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 56, aliyefutwa kazi hivi karibuni na klabu ya Manchester United ya Uingereza, alikuwa kocha pia wa Real Madrid mwaka 2010 hadi 2013.