Moyes atimuliwa United, FC Cologne yerejea Bundesliga
22 Aprili 2014Ikitangaza kuondoka kwa Moyes katika taarifa fupi iliyotolewa muda mfupi baada ya wafanyakazi kuwasili katika uwanja wa mazoezi wa Carrington, MANU ilimshukuru kocha huyo raia wa Scotland kwa kazi kubwa, uaminifu na uadilifu alivyovionyesha akiwa katika nafasi hiyo. Mapema, magazeti yalikuwa yameripoti kuwa kibarua cha Moyes kilikuwa kimeota nyasi, baada ya wamiliki wa klabu hiyo, familia ya Glazer kutoka Marekani kushindwa na uvumilivu na kuamua kumtema.
Moyes, ambaye anatimiza umri wa miaka 51 Ijumaa hii, aliteuliwa kwa mapendekezo ya Mscoti mwenzake Ferguson, aliestaafu mwishoni mwa msimu uliyopita baada ya kuitumikia klabu ya Manchester United kwa miaka 26. Ferguson aliiongoza klabu hiyo katika ushindi taji lake la 13 chini ya uongozi wake, na la 20 kwa jumla. Kuondoka kwa ghafla kwa Moyes kumerejesha kumbukumbu za kipindi kibaya ilichokipitia klabu hiyo ya Old Trafford kati ya mwaka 1969 na 1971, kufuatia kustaafu kwa Matt Busby, baada ya kuiongoza kwa miaka 24.
Mrithi wake aliemchagua mwenyewe Wilf McGuiness alidumu klabuni kwa miezi 18 tu kabla ya Busby kurudi na kuchukuwa tena mikoba yake. Lakini hakuna uwezekano kwa Ferguson kuacha kazi yake ya sasa inayompatia kipato kikubwa kama mzungumzaji kwenye tafrija na mshauri wa kibiashara kurudi Manchester United.
Mdachi Louis van Gaal kumrithi?
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, United wamezungumza na Mdachi Louis van Gaal, ambaye atajiuzulu kama kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi baada ya mashindano ya kombe la dunia nchini Brazil mwezi Juni na Julai. Mchezaji nguli wa kati Ryan Giggs mwenye umri wa miaka 40, ambaye amekuwa msaidizi wa Moyes, amepewa majukumu ya kuiongoza klabu hiyo katika michezo iliyosalia msimu huu.
Moyes ambaye alikuwa kocha wa klabu ya Everton kwa misimu 11 bila kushinda taji alipewa mkataba wa miaka 6 na Manchester United lakini wamekuwa wakitoka kwenye mgogoro mmoja baada ya mwingine. Kipigo cha kushtua cha magoli 2-0 dhidi ya Everton siku ya Jumapili ndiyo ulikuwa mwisho wa subira kwa familia ya Glazer, huku Manchester United inayoshika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ikishindwa kufuzu kwa mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 1995-96.
FC Cologne yarejea katika Bundesliga
Wakati hali ikiwa ni ya kutoelewana katika uwanja wa Old trafford, klabu kongwe ya jiji la Cologne nchini Ujerumani, FC Cologne ilijihakikishia kurudi katika ligi ya dara la kwanza -ligi kuu- Bundesliga msimu ujao, baada ya kushinda taji la ligi ya daraja la pili siku ya Jumatatu.
Klabu hiyo inayonolewa na kocha Peter Stoeger ilitoka nyuma na kuishinda Bochum magoli 3-1 mbele ya mashabiki waliofurika katika uwanja wao wa nyumbani wa Rheinenergiestadion, wenye uwezo wa kubeba watazamaji 50,000. Ushindi huo uliipa FC Cologne tofauti ya pointi 10 mbele ya klabu ya pili kimsimamo ya Gruether Fuerth, huku zikiwa zimesalia mechi tatu msimu kumalizika.
Kihistoria, FC Cologne ni moja ya klabu kubwa zaidi nchini Ujerumani, lakini miaka ya hivi karibuni imekuwa katika mkosi wa kupanda na kushuka daraja na mwisho kucheza daraja la kwanza ilikuwa katika msimu wa 2011-2012.
FC Cologne iliwahi kuwa bingwa wa Ujerumani mara tatu, ukiwemo ubingwa wa ufunguzi wa ligi kuu ya Bundesliga mwaka 1963-64, lakini taji lao muhimu la mwisho lilikuwa ni kombe la Ujerumani mwaka 1983.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman