1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atakuwa kiongozi mpya nchini Uingereza?

12 Julai 2022

Aliyekuwa waziri wa fedha Rishi Sunak atajwa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kumrithi waziri mkuu Boris Johnson aliyelazimishwa kujiuzulu

Boris Johnson im UK Parlament
Picha: Jessica Taylor/UK Parliament/AP/picture alliance

Nchini Uingereza harakati za kuwania nafasi ya waziri mkuu zimeshika kasi wagombea mbali mbali wakijinadi kupitia sera zao. Kuna wagombea 11 wanaotaka kuchaguliwa kukiongoza chama cha Conservative na hatimae kutwaa kiti cha waziri mkuu  baada ya Boris Johnson kulazimishwa wiki iliyopita  kutangaza kujiuzulu.

Picha: Jessica Taylor/UK Parliament/AP/picture alliance

Wagombea wote wanaotaka kurithi kiti cha waziri mkuu kinachoachwa na  Boris Johnson wameshajitupa kikamilifu uwanjani kuanzia leo katika mpambano wa mwanzo kabisa  ambao ni kutafuta uungaji mkono wa kutosha wa wabunge wenzao katika chama cha Conservative na kupitishwa.

Shughuli ya uteuzi ilianza mapema kabisa leo asubuhi na kumalizika jioni hii. Na mgombea atahitaji kuungwa mkono na alau wabunge 20 wa chama hicho cha kihafidhina ili kupata nafasi ya kuingia kwenye orodha ya watakaopigiwa kura ya mchujo  ya duru ya pili ambayo itafanyika kesho Jumatano.

Wenye nafasi ya kushinda

Mpaka kufikia sasa ni wagombea watatu tu kati ya 11 waliojitokeza ndio waliokwisha vuka kiunzi cha kuungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge inayohitajika,nao ni aliyekuwa waziri wa fedha Rishi Sunak,waziri wa biashara Penny Mordaunt na mbunge Tom Tugendhat.Wengine ambao pia inaelezwa wanaweza kuvuka kiunzi hicho ni pamoja na waziri wa mambo ya nje Liz Trusss,waziri wa fedha wa sasa Nadhim Zahawi na aliyekuwa waziri wa afya Jeremy Hunt.

Wagombea wote wanapambana kumrithi Boris Johnson aliyejiuzulu kama kiongozi wa chama hicho cha Consertavive wiki iliyopita kufuatia uasi mkubwa ulioibuka ndani ya chama hicho uliochochewa na miezi kadhaa ya kashfa za kimaadili moja baada ya nyingine dhidi ya waziri mkuu Johnson ambaye anaendelea kubakia katika nafasi hiyo kwa muda hadi atakapopatikana kiongozi mpya wa chama.

Picha: Alberto Pezzali/AP/picture alliance

Anayetajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa mpaka wakati huu ni aliyekuwa waziri wa fedha Rishi Sunak ambaye leo ameanza kampeini zake kwa kuahidi kuwa na serikali ya uwazi.Waziri wa uchukuzi Grant Shapps ni mgombea wa mwanzo kujiengua kwenye kinyang'anyiro hiki na kutangaza kumuunga mkono Sunak ambaye kimsingi kujiuzulu kwake ndiko kulikochochea sekeseke la mawaziri wengine wengi na wabunge nao kujiuzulu.

Wagombea wengi akiwemo Penny Mordaunt, naibu waziri wa biashara ambaye pia anatajwa kuwa na nafasi nzuri, wanajinadi kwa karata ya kupunguza kodi wakichaguliwa lakini Sunak amechagua kujinadi kama mgombea makini,anayeahidi uongozi wa ukomavu,wenye kuzingatia ukweli na sio wa hadithi za kubuni.- Anaungwa mkono pia na naibu waziri mkuu Dominic Raab.Waziri wa mambo ya nje Liz Truss hii leo nae amepata uungwaji mkono wa mawaziri wawili walioko karibu na Boris Johnson,Nadine Dorries na Jacob Rees-Mogg,wote ni wakosoaji wa Sunak.

Kitakachofanyika ni kwamba kiongozi mpya atachaguliwa katika duru mbili za uchaguzi zitakazowahusisha wabunge  358 wa chama cha Conservative watakaopiga kura na kuwachuja wagombea mpaka watakapopatikana wawili. Wagombea hao wawili baadae watapigiwa kura na wanachama wote wa chama hicho kote nchini ambao ni 200,000.

Picha: Dan Kitwood/Getty Images

Duru ya mwanzo ya mchujo ni kesho jumatano na wagombea watakaoshindwa kuuungwa mkono na alau wabunge 30 watafungasha virago na duru nyingine itafanyika alhamisi.Mshindi atakayekuwa waziri mkuu mpya atatangazwa Septemba 5.

Wakati hayo yakijiri Chama kikuu cha upinzani cha Labour kinajiandaa leo kupeleka bungeni muswaada wa kura ya kutokuwa na imani na serikali kujaribu kulazimisha waziri mkuu Boris Johnson aondoke kwenye nafasi hiyo maramoja.Kura hiyo itapigwa kesho jumatano japokuwa pamoja na baadhi ya wahafidhina kuonesha wasiwasi na waziri mkuu Johnson kuendelea kuwepo,uwezekano ni mdogo kwamba watauunga mkono muswaada huo.