1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa amani wa Gaza wapongezwa kimataifa

14 Oktoba 2025

Viongozi mbalimbali wa dunia wamepongeza na kuunga mkono mpango mya wa amani kuhusu mzozo wa Gaza wakionesha matumaini ya kufikiwa kwa hali ya utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Sharm el-Sheikh 2025 | Mkutano wa amani kuhusu mzozo wa Gaza
Mkutano wa amani kuhusu mzozo wa Gaza uliofanyika nchini Misri: 13.10.2025Picha: Yoan Valat/REUTERS

Mkutano wa amani kuhusu mzozo wa Gaza uliofanyika Jumatatu (13.10.2025) nchini Misri umewezesha kusainiwa kwa makubaliano yanayotazamiwa kurejesha utulivu huko Mashariki ya Kati baada ya miaka miwili ya vita vya umwagaji damu kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas.

Mkutano huo uliofanyika katika mji wa Sharm el-Sheikh, ulihudhuriwa na viongozi zaidi ya 20 kutoka mataifa ya Ulaya, Kiarabu na Asia. Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na marais wa Misri, Uturuki na Emir wa Qatar walitia saini tamko la pamoja la  kudumisha urithi wa amani."

Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya usalama, uongozi wa Gaza na mpango wa ujenzi mpya wa ukanda huo ulioharibiwa vibaya na vita, huku viongozi wengi wakisisitiza haja ya misaada ya kibinaadamu kufikishwa kwa haraka kwa Wapalestina. Kuanzia jana, malori zaidi ya 300 yalianza kuingizwa  Gaza kupitia vivuko vya Al-Awja na Kerem Shalom.

Viongozi mbalimbali wa dunia akiwemo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wametaja kuunga mkono na kupongeza juhudi hizo za kimataifa wakisema kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo ni ishara ya matumaini mapya kwa eneo hilo.

Biden na Clinton wampongeza Trump 

Marais wa zamani wa Marekani: Kutoka kushoto: Barack Obama, Joe Biden na Bill ClintonPicha: Elisabeth Frantz/REUTERS

Katika hatua ya nadra, marais wa zamani wa Marekani kutoka chama cha Democratic Bill Clinton na Joe Biden wamempongeza  Trump  kwa kufanikisha mpango huo wa amani uliowezesha hapo jana kuachiliwa kwa mateka wote wa Israel na mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

Hatua hiyo imeleta matumaini kwa Wapalestina waliokubwa na vita vibaya kama anavyoeleza Saeed Al-Banna raia wa Gaza:

"Naunga mkono juhudi zozote zitakazoleta usalama, utulivu na kufufua uchumi ili kuwapa watu faraja kwani wananchi wamechoka. Juhudi zozote zile hata kama ni dogo zitazaa matunda kwa uwezo wake Mola, kwa sababu tumechoka na tunataka kulea watoto wetu."

Hata hivyo, vipengee kadhaa bado vinazua utata, ikiwa ni pamoja na suala la suluhisho la mataifa mawili. Kuhusu hilo Trump amesema hivi leo kuwa atashirikiana na mataifa mengine na baadaye ataamua anachofikiri ni sahihi katika suluhisho la muda mrefu la  mzozo huo kati ya Israel na Palestina huku Mfalme Abdullah II wa Jordan akitahadharisha kusipokuwepo mchakato wa amani utakaowezesha uwepo wa taifa huru la Palestina, basi Mashariki ya Kati "itaangamia."

Hayo yakiarifiwa, Wapalestina sita wameuawa Jumanne huko Gaza baada ya kufyetuliwa risasi na jeshi la Israel lililodai kwamba hatua hiyo ilikuwa kujihami dhidi ya washukiwa waliokiuka makubaliano ya awali na walijaribu kuvisogelea vikosi vyake vilivyopo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

// AP, DPA, RTR, AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW