Mpango wa amani ya Syria waidhinishwa
20 Desemba 2015Hii ikiwa ni hatua ya kipekee ya iliyoonesha umoja miongoni mwa mataifa makubwa katika mzozo ambao umesababisha kupotea kwa maisha ya watu zaidi ya robo milioni.
Azimio hilo linatoa ridhaa kwa mpango uliojadiliwa hapo kabla na Umoja wa Mataifa mjini Vienna ambao unatoa wito wa kusitishwa mapigano, mazungumzo baina ya setikali ya Syria na upinzani, na muda wa miaka miwili ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa Kitaifa na kisha kufanya uchaguzi.
Mkwamo bado upo
Lakini vikwazo katika kumaliza karibu miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe bado vinaendelea kuleta mkwamo, ambapo hakuna upande katika mzozo huo ambao unaweza kupata ushindi wa wazi kupitia njia za kijeshi.
Licha ya makubaliano yao, mataifa makubwa yanatofautiana mno juu ya nani huenda akawakilisha upinzani pamoja na hali ya baadaye ya rais Bashar al-Assad.
"Baraza hili linatoa ujumbe wa wazi kwa wale wote wanaohusika kwamba muda ni sasa wa kusitisha mauaji nchini Syria na kuweka msingi kwa ajili ya serikali ambayo umma unaoteseka kwa muda mrefu katika nchi hiyo iliyotumbukia katika mzozo unaweza kuiunga mkono," waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ameliambia baraza hilo lenye wanachama 15 baada ya kura hiyo.
Azimio hilo pia linatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuwasilisha katika baraza hilo uwezekano wa kuangalia usitishaji mapigano katika muda wa mwezi mmoja.
Mazungumzo kati ya serikali ya Syria na upinzani yanapaswa kuanza mapema Januari, azimio hilo limesema, licha ya kuwa Kerry amesema katikati hadi mwisho wa Januari huenda ni muda muafaka zaidi. Pia azimio hilo limeidhinisha mapambano zaidi dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu ambao wamekamata maeneo makubwa nchini Syria na nchi jirani ya Iraq.
Azimio hilo limekuja baada ya Urusi na Marekani kufikia makubaliano ya waraka. Mataifa hayo mawili yamekuwa na mtazamo tofauti kuhusiana na kile kinachopaswa kutokea nchini Syria , ambako wanamgambo wa Dola la Kiislamu wanadhibiti eneo kubwa ambalo serikali za mataifa ya magharibi wanashuku limekuwa eneo linalotumiwa kwa mashambulizi ya kundi hilo dhidi ya mataifa ya magharibi na Urusi.
Mustakabali wa rais Assad bado haujajulikana
Kerry ameweka wazi kwamba kuna tofauti bado kuhusu hali ya baadaye ya Assad , mshirika wa karibu wa Urusi na Iran ambae mataifa ya magharibi yanataka aondoilewe, pamoja na suala la makundi gani ya Syria yatakuwa na viti katika meza ya duara katika mazungumzo pamoja na serikali.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amesema mazungumzo baina ya serikali ya Syria na upinzani yatafanikiwa tu iwapo kutakuwa na uhakikisho wa kweli kuhusiana na kuondoka kwa Assad.
Balozi wa Syria Bashar Ja'afari amesema serikali ya Assad iko tayari kushiriki katika mazungumzo hayo kwa nia njema kabisa.
Makubaliano katika azimio hilo yamekuja baada ya mkutano wa kile kinachofahamika kama kundi linalotoa usaidizi kwa Syria katika hoteli ya Palace mjini New York.
Usitishaji wa mapigano
Muongozo kuhusu Syria , ambao pia unatoa wito kwa usitishaji wa mapigano nchi nzima ambao utahusisha pia Dola la Kiislamu, Nusra Front na baadhi ya makundi ya wanamgambo, yalifanyiwa kazi hapo kabla katika duru mbili za mazungumzo katika ngazi ya mawaziri mjini Vienna.
Wanadiplomasia wamesema tatizo kubwa katika majadiliano kuhusu azimio hilo yaliyohusisha wasi wasi wa Urusi na Iran juu ya vipi kuliangalia kundi la makundi ya wapinzani ambao watajiunga na mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa pamoja na serikali ya Syria.
Javad zarif aliandika katika gazeti la Guardian siku ya Ijumaa kwamba ni kitu cha kushangaza sana, kwamba wale ambao wamewanyima watu wao wenyewe haki za msingi kabisa za demokrasia...sasa wamejitangaza kuwa mabingwa wa demokrasia nchini Syria.
Mkutano wa Riyadh umekubaliana kuunda sekretariati yenye wajumbe 34 kuangalia mazungumzo ya amani , na kamati hiyo pia itachagua watu kutoka upande wa upinzani watakaoshiriki katika mazungumzo hayo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Isaac Gamba